Kizazi njia panda: angalia nyuma ya pazia
Ni watu gani wanaoigiza katika mchezo wa redio Kizazi njia panda? Hapa utapata kuwajua. Baadhi ya wahusika utakuwa umewafahamu kwa sasa, lakini kuna wapya pia ambao tutawatambulisha hivi karibuni katika awamu ya tatu.
Mchezo ulikoigizwa
Je, wewe ni shabiki wa Kizazi njia panda? Umefuatilia kwa karibu kila kipindi na bado unayo hamu ya kufahamu zaidi? Basi ungana nasi na tutakuonyesha wahusika wa mchezo huu. Mabingwa wa Bongo Academy uliokutana nao katika mchezo huu wa redio wamepewa sauti na waigizaji jijini Dar-es-Salaam, Tanzania.
Trudy
Huyu hapa mwenye nguo nyekundu ni Deborah Dickson, aliyeigiza kama Trudy, rafiki yake Mercy, katika awamu ya kwanza na ya pili ya mchezo huu. Trudy ni miongoni mwa mashabiki wa mwanzo kabisa wa kijana mmoja aliyejiunga na shule hiyo, kijana anayetoka nchi jirani ya Laboria…
Dan
Kijana huyo ni Dan Kanyama, alieigizwa na Collins Msonga. Kama umeitambua sura yake, basi ni kwamba umeifuatilia mikanda ya vidio aliyoinakili wiki kwa wiki akiwa nchini Kisimba - ili kujieleza kwa marafiki zake nyumbani Laboria. Lakini hima tu baba yake, mmiliki wa kampuni kubwa, asipate kujua!
Niki
Macray Rusasa ndiye anayeigiza kama Niki Jumbe katika mchezo wa Kizazi njia panda. Kwa upande wake, Niki hana baba tajiri. Lakini hayo hayamzuii kushindana na Dan ili kumvutia msichana mwenye nasaba ya kimasikini lakini mwenye akili nyingi.
Mercy
Jina lake ni Mercy Msoto. Mwigizaji ni Rachel Kubo (kulia). Katika awamu ya tatu, Mercy anajenga urafiki na Tina Wigo (Mwasiti Hussein, kushoto). Wanakutana kwenye chuo kikuu ambako wote wawili wamejiandikisha kwa masomo ya uandishi habari.
Tina
Miaka mitatu imepita tangu siku tulipowasindikiza huko shuleni Bongo Acadamy. Lo! Bado ni wanafunzi katika mambo mengi, na maisha yenyewe yatazidi kuwafunza! Tina ni nyota wetu wa awamu ya tatu. Kila baada ya wiki moja atatueleza aliyoyapitia katika mkanda wa vidio.
Lulu, Banda na Kadu
Bila shaka, Lulu Msoto, mama yake Mercy, na ndugu zake Banda na Kadu watasikika tena katika awamu hiyo mpya. Anayeigiza kama Lulu ni Betty Kazimbaya. Badru Bilal ndiye tunayemzoea kama Banda na Kadu anaigizwa na Nashiri Juma.
Mtunzi wa mchezo
Hakuna mchezo wa kuigiza bila ya mtunzi. Jina lake James Muhando. Lakini kazi yake haiishii pale. James ambaye mwenyewe amezoea kazi ya uigizaji anawapa ushauri nyota wetu wa Kizazi njia panda kila inapohitajika. Huyu hapa akizungumza na Mwasiti Hussein - ama tuseme Tina.
Kutoka Bonn
Kwinigineko, aliyesimamia uigizaji wa mchezo huu wa redio ni Grace Kabogo, mmoja wa wanahabari wa idhaa ya kiswahili ya Deutsche Welle. Alifunga safari mjini Bonn pamoja na fundi mitambo Götz Bürki ili kuifanikisha kazi hiyo. Na bila shaka walifurahia!