Kongamano la madini Tanzania fursa kwa Afrika
25 Oktoba 2023Kongamano hilo la siku mbili ni uwanja unaotumiwa na nchi mwenyeji na mataifa mengine Jirani kuilezea hadhira ya kimataifa namna sekta ya madini inavyopewa kipaumbele katika wakati huu ambako inatizamwa kuwa kiungo muhimu cha kukuza uchumi.
Mwenyeji Tanzania amesema sekta ya madini bado inaendelea kupanuka na kwamba ikiwa ndiko nyumbani kwa madini pekee yanayopatikana ulimwenguni Tanzanite, imedhamiria kushirikiana na wawekezaji wa kigeni kuinua sekta hiyo kwa ajili ya kunufaisha pande zote.
Soma pia:Angola, DRC zalenga ukarabati wa reli muhimu kukidhi kiu ya madini duniani
Kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika yanayokabiliwa na ufinyu wa teknolojia za kisasa kwa ajili ya kuendesha miradi mikubwa ya utafutaji wa madini, Waziri wake wa madini Antony Mavunde amewahakikishia wawekezaji wa kigeni na wazawa kwamba suala hilo linakwenda kuwa historia katika siku chache za usoni.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Waziri wa madini wa Malawi, Monica Changamamuno alisema nchi yake imepitia sera zake na kuziweka katika mazingira yanayoweza kuwafanya wawekezaji wa kigeni kuwa salama na kunufaika na uwekezaji wao.
AlisemaMalawi imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha na kuboresha nishati ya umeme kwa kuanzisha miradi mikubwa itayofanikisha uwekezaji unaokusudiwa.
Malawi: Tunahitaji wawekezaji katika sekta ya madini
Malawi inawaalika wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta kubwa ya madini…najua kuna makampuni mengi yanawekeza hapa, na hakika itakuwa rahisi kupanua uwekezaji wenu.
Kongamano hilo ambalo pia limewajumuisha wataalamu wa masuala ya madini pamoja na wawekezaji wa kimataifa linajadili ni kwa kiasi gani sekta hiyo inayotajwa kuwa kiini cha migogoro katika baadhi ya maeneo inavyoweza kutoa mchango kukuza mataifa ya Afrika.
Soma pia:Tanzania yasaini mikataba ya madini ya nadra na makampuni ya Australia
Naibu Waziri mkuu wa Tanzania aliyekuwa mgeni rasmi, Dk Dotto Biteko alisema serikali itaendelea kutilia msukumo ajenda ya uwekezaji katika maeneo ya utafutaji madini bila kusahau uimarishaji wa sekta ya nishati ya umeme.
Kongamano hilo linafanyika huku kukiwa na msukumo mpya kuhusu uanzishwaji wa mkakati wa kusaka madini yanayopatikana baharini.