Korea Kaskazini, siasa za matope za AfD magazetini
17 Mei 2018Mhariri wa gazeti la Volksstimme la mjini Magdenburg anazungumzia kitisho cha Korea Kaskazini kufuta mkutano wa kilele kati ya kiongozi wake Kim Jong Un na Rais wa Marekani Donald Trump. Mhariri huyo anasema hatua hiyo inaacha hitimisho moja tu - kwamba anataka kupandisha gharama za kuachana na mpango wake wa nyuklia na kutuliza mzozo katika rasi ya Korea.
Anasema mpaka sasa mtawala huyo wa Pyongyang ndiye alikuwa na karata nzuri katika mazungumzo ya nyuklia. Amempa ushindi wa kidiplomasia rais wa Marekani Donald Trump kwa hatua yake ya kukubali kufanya naye mazungumzo. Lakini Kim anaweza kujikanganya kwa urahisi.
Mshirika wake pekee na wa mwisho China, inataka mchakato wa kuiondolea silaha za nyuklia rasi ya Korea ufanyike sasa hivi. Kim naye anaonyesha kutaka hilo, lakini bila kutangaza kuachana kabisaa na mpango wake wa nyuklia. Hivyo anaweza sitoke.
Naye mhariri wa gazeti la Südwest-Presse la mjini Ulm, anasema ni jambo la kusuburi kuona iwapo kweli Kim yuko tayari kuachana kabisaa na mpango wake wa silaha za nyuklia. Anasema kwa sasa unaweza kusema kuna maendeleo - ambayo ni msingi wa mazungumzo. Uzowefu hata hivyo unaonyesha kwamba mazungumzo ya upunguzaji wa nguvu za silaha ni biashara ngumu na inayochukuwa muda mrefu. Vikwazo bado vipo vingi tu.
AfD na siasa za matope Ujerumani
Mhariri wa gazeti la Oberhessische Presse ameandika juu ya mashambulizi ya kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AFD Alice Weidel, dhidi ya kansela Angela Merkel wakati wa mjadala wa kwanza wa wazi katika muhula wa sasa wa bunge la Ujerumani Bundestag.
Anasema Weidel na wenzake hawasumbuliwi na kutokujali kwa Merkel wanapomshambulia kama wanavyofanya kwa makundi mengine. Na hilo ni hatari kwa misingi kadhaa. Kwa upande moja, wabunge wa AFD hawajaelimishwa kuhusu utamaduni uliowekwa wa mijadala mpaka sasa.
Pili, kundi la AFD linaweza kucheza karata ya mwathirika kila wanapotakiwa kuheshimu utaratibu, na kupitia mchezo huu, wafuasi hao wa siasa kali za mrengo wa kulia wanaweza demokrasia ya mfumo wa bunge.
Mwisho kabisaa na pengine hatari kubwa zaidi, uharibu wa vikao vya bunge kama cha jana, umeacha maeneo yasiyo ya upendo kama vile "wasio na manufaa", "wasichana wenye mitandio", alau yakikubalika kwa watu ambao bado wanadhani wanaweza kusema tu lolote linalowajia kichwani.
Siku ya kupambana na chuki dhidi ya mashoga
Mhariri wa gazeti la Der Neue Tag la mjini Weiden ameandika juu ya siku ya kimataifa ya kupinga chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja. Anataja kisa cha afisa wa Chechnya alieulizwa na mwandishi wa habari wa Canada kuhusu kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa mashoga katika Jamhuri ya Urusi. Alimjibu kwamba "hatuna watu wa namna hiyo, siyo watu na kama wapo, wachukuwe nyumbani kwenu Canada ili damu yetu itakaswe." Hilo halimuachi mpiganaji huyo pekee yake, anasema mhariri huyo na kuongeza kuwa
Katika mataifa 72 sheria dhidi ya mashoga zinatumika. Wapenzi wa jinsia moja wanakabiliwa na adhabu ya kifo katika mataifa 13 ya Kiafrika na Asia. Lakini hata hapa Ujerumani, mashoga na wasagaji hawawezi kujiskia salama kikamilifu. Kila siku kuna kisa kinachoripotiwa cha mashambulizi yayanyochochea na chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, idadi ya visa hivyo iko juu.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche zeitungen
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman