LRA bado ina nguvu licha ya mashambulizi ya AU
16 Januari 2015Magari ya kijeshi yanayotimua vumbi kutoka barabara chafu karibu na kijiji cha Nzako katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hayaonekani kuwashangaza wenyeji walioko kandoni mwa barabara hiyo wakitafuta kivuli cha miti. Vikosi vya wanajeshi wa Umoja wa Afrika viko katika eneo hilo la kusini mwa nchi, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kuwalinda raia kutokana na mashambulizi ya kundi la Lord's Resistance Army, LRA.
Wanajeshi hao - wengi wao kutoka Uganda, Jamhuri ya Congo na Sudan Kusini - wakisaidiwa na Marekani - wamekuwa wakijaribu kuwasaka masalia wa LRA tangu mwaka 2012 katika eneo hilo lenye misitu mikubwa. Bado kunaaminika kuwepo na mamia kadhaa ya wapiganaji wa kundi hilo, lililoorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, ingawa wanajeshi wa Umoja wa Afrika wameripotiwa kupata mafanikio muhimu.
Kukamatwa kwa makamanda wake
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, vitendo vya utekaji nyara katika vijiji vya eneo hilo vinavyofanywa na LRA vimepungua kwa nusu katika miaka ya karibuni. zaidi ya hayo, makamanda sita wa LRA wamekamatwa, wa karibuni zaidi akiwa Dominic Ongwen, moja wa makamanda muhimu zaidi, ambaye atakabidhiwa kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague, nchini Uholanzi.
Pamoja na hayo, bado hakuna dalili ya kukamatwa kwa kiongozi wa kundi hilo Joseph Kony. Na wala haijulikani wazi amejificha katika nchi gani pamoja na wafuasi wake waaminifu. Kilicho wazi ni kwamba waasi wa LRA waliojihami kwa silaha nzito huibuka mara kwa mara kutoka msituni na kufanya mashambulizi kawenye vijiji, hasa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Waasi hao wamekivamia kijiji cha Nzako mara tatu.
Mbinu za LRA zawachanganya AU
Kiongozi wa kijamii wa kijiji hicho Mahmad Ganda, anasema LRA walivamia soko la kijiji, wakachukuwa kila kitu, wakauwa watu kadhaa wakiwemo wanajeshi waliowekwa kutoa ulinzi. Msemaji wa vikosi vya Uganda katika Jamhuri ya Afrika ya Kati Robert Kamara, anasema LRA inajaribu kujinusuru kwa njia zozote zile, na bado wana uwezo wa kuendesha operesheni zao katika mazingira magumu zaidi. LRA wana uwezo wa kuchuma matunda, kulina asali, kuvua samaki na kupata nyama kutoka msituni.
Kamara anasema ni vigumu sana kwao kuwafuatilia. " Njia pekee ni kutembea kwa miguu na kuishi msituni kama wanavyofanya kwa wiki kadhaa, anasema huku akiangalia msitu mzito kutokea dirisha la helikopta ya kijeshi. Mwaka 1987, LRA ilianza kufanya ukatili kaskazini mwa Uganda, ikiwateka maelfu ya watoto kwa miaka kadhaa na kulwalazimisha kuwa wanajeshi.
Hofu ndiyo zana yao kuu
Ongweni alikuwa moja wapo. Alitekwa na waasi akiwa na umri wa miaka 10 na kuingizwa jeshi, na kufanya juhudi hadi kufikia ngazi ya kamanda wa juu katika kundi hilo. Mwaka 2005, kundi hilo liliondoka nchini Uganda, na tangu wakati huo limekuwa likifanya utekaji nyara katika eneo la mpakani mwa DRC, Sudan Kusini na Kongo. Karibu watu milioni mbili wameyakimbia makaazi yao katika eneo hilo.
Hofu ndiyo zana yenye nguvu zaidi inayotumiwa na waasi hao, ambao wanahalalisha vita vyao kwa misingi ya dini. Katika eneo linalozunguka Obo, mbali kabisaa kusini-mashariki na Jamhuri ya Afrika ya Kati, karibu makaazi yote yameisha, na wakulima wanapanda mazao katika maeneo yanayolindwa na Umoja wa Afrika tu.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae
Mhariri: Saumu Yusuf