Macron aendeleza juhudi kuzima mzozo Ukraine
8 Februari 2022Ziara ya Rais Macron inakuja baada ya mazungumzo na rais wa Urusi Vladmir Putin yaliodumu kwa masaa kadhaa, kumalizika bila muafaka wa dhahiri.
Macron amekutana na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensnky, wakati ambapo wasiwasi ukiongezeka juu ya uwezekano wa uvamizi wa Urusi.
Taifa hilo limepeleka wanajeshi zaidi ya 100,000 karibu na mipaka ya Ukraine, lakini linasisitiza kuwa halina mipango ya kuishambulia nchi hiyo.
Kremlin inasema inataka uhakikisho kutoka mataifa ya Magharibi kwamba NATO haitoikubalia uanachama Ukraine na mataifa mengine yaliokuwa sehemu ya Muungano wa Kisovieti, kwamba isitishe uwekaji wa zana za kivita katika eneo hilo, na kuondoa vikosi vyake kutoka eneo la Ulaya Mashariki - madai ambayo Marekani na NATO imeyakataa na kuyataja kuwa yasio na mashiko.
Mazungumzo ya Macron na Putin siku ya Jumatatu yalidumu kwa zaidi ya masaa matano, na kiongozi huyo wa Ufaransa aliwaambia waandishi habari kwamba hakutarajia Putin kutoa ishara zozote, lakini lengo lake lilikuwa kuzuwia kuongezeka kwa mzozoz huo na kufungua mitazamo mipya, lengo ambalo lilifiwa.
Putin alisema baada ya mkutano huo kuwa Marekani na NATO wamepuuza madai ya serikali yake, lakini aliashiria utayari wake wa kuendelea na majadiliano.
Soma pia: Marekani yatuma wanajeshi, mzozo wa Ukraine ukizorota
Putin alionya kuwa hatua ya kuipatia Ukraine uanachama wa NATO inaweza kusababisha vita kati ya Urusi na muungano huo, endapo Kyiv itachukuwa hatua za kurejesha rasi ya Crimea, ambayo Moscow iliiteka mwaka 2014.
Alisema hatua hiyo itaziburuta nchi za Ulaya katika mzozozo wa kijeshi na Urusi, ambapo hakutakuwa na washindi.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema hakuna matarajio ya Ukraine kujiunga na NATO katika muda wa karibuni, lakini yeye na mataifa wanachama wa NATO na NATO yenyewe wanakataa kuondoa uwezekano wa Ukraine kujiunga na muungano huo huko mbeleni.
Soma pia: Wajumbe wa Ukraine na Urusi wakutana Paris
Ziara ya Macron mjini Kyiv, inajiri wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, akizuru mkoa wa mashariki mwa Ukraine wa Donbas, ambako amepatiwa maelezo kuhusu hali ya kibinadamu na kijeshi. Serikali ya Ukraine imekuwa katika mzozo wa kivita na waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa taifa hilo tangu mwaka 2014.
Rais Macron anatarajiwa pia kukutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Poland Andrzej Duda mjini Berlin ili kuzingatia sauti za Ulaya Mashariki na misimamo katika kuishughulikia Urusi, kwa sababu huko nyuma, rais huyo wa Ufaransa ameshthumiwa kuwa karibu sana na Urusi.
Waziri Mkuu wa Romania Vasile Dincu amefahamisha kuwa kundi la kwanza la wanajeshi wa Marekani limewasili nchini humo kuimarisha kikosi cha NATO kwenye ngome yake ya Mashariki.
Dincu amewaambia waandishi habari kuwa wanajeshi 100 wamewasili kushughulikia masuala ya lojistiki.
Chanzo: AFP, AP/DW