Maelfu waandamana kuhusu mabadiliko ya tabia nchi
29 Novemba 2019Maelfu ya watu nchini Australia na nchi kadhaa za Ulaya wameungana na wengine ulimwenguni kuandamana ili kushinikiza hatua zaidi zichukuliwe kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kwa lengo la kuwataka viongozi wa kisiasa kupata masuluhisho ya dharura katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi utakaonza wiki ijayo nchini Uhispania.
Hapa nchini Ujerumani, maandamano hayo kwa jina la "Ijumaa kwa ajili ya Mustakabali" yamefanyika katika zaidi ya miji 500, ukiwemo mji mkuu Berlin ambapo zaidi ya waandamanaji 50,000 wameshiriki.
Miongoni mwa matakwa ya waandamanaji nchini Ujerumani ambao wanakadiriwa kufikia 100,000 ni kuachana kabisa na matumizi ya nishati ya visukuku, kuzima robo ya vituo vya kuzalisha nishati kutokana na makaa ya mawe na mahitaji ya nishati ya Ujerumani yatimizwe kutumia vyanzo vya nishati salama kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2035.
Mioto ya misitu Australia kutokana na mabadiliko ya tabia nchi?
Nchini Australia, wanaharakati pamoja na wanafunzi waliandamana mbele ya makao makuu ya chama tawala cha kiliberali. Walielekeza upinzani wao kwa Waziri Mkuu Scott Morrison ambaye amekanusha uhusiano wowote wa sera ya serikali yake kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na mioto ya misitu ambayo imekuwa ikiteketeza baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Isabella D' Silva ambaye ni mmoja wa waandamanaji Australia amesema: "Tunahitaji haki sasa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ili kuleta mabadiliko si ulimwenguni, lakini katika nyumba zetu. Ikiwa hatujafanya hivyo katika majumba yetu, katika jamii zetu, ni vipi tutaeneza haki ulimwenguni kwote?"
Athari za mabadiliko ya tabia nchi Japan
Nchini Japan, mamia ya watu wameandamana mjini Tokyo kuonesha uungaji wao mkono kwa madai hayo. Katika miaka ya hivi karibuni, Japan tayari imeathiriwa na viwango vya juu vya joto na vimbunga vya mara kwa mara kikiwemo kimbunga Hagibis kilichopiga maeneo ya kati, na kaskazini mashariki na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Mwanaharakati mdogo wa mabadiliko ya tabia nchi kutoka Sweden, Greta Thunberg, ambaye alitarajiwa kujiunga na waandamanaji mjini Lisbon, alikosa kujiunga na wenzake baada ya boti yake kukumbwa na upepo mkali katika Bahari ya Atlantiki akitokea New York, na hivyo kuchelewesha safari yake. Hata hivyo waandaaji wa maandamano hayo nchini Ureno walisema wanatarajia maelfu ya watu kujitokeza
Mkutano wa COP 25
Maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo wajumbe kutoka takriban nchi 200 wanajiandaa kukutana mjini Madrid, Uhispania. Washiriki wa mkutano huo wa mabadiliko ya tabia nchi, COP25, wanatazamiwa kujadili sheria za wazi kuhusu namna ya kutekeleza matakwa ya maafikiano ya makubaliano ya Paris mwaka 2015 kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Hapo jana, bunge la Ulaya lilipiga kura ya kutangaza mazingira kuwa suala la dharura kote katika Umoja wa Ulaya.
Vyanzo: DPAE, AFPE