Mafuriko yaacha watu 200,000 bila makazi Somalia
14 Mei 2023Matangazo
Afisa wa eneo hilo aliliambia shirika la habari la AFP kwamba athari hizo zimetokana na kupasuka kwa kingo za Mto Shabelle, hali iliyosababisha pia barabara kufurika maji. Wakazi wa mji wa Beledweyne katika mkoa wa Hiran walilazimika kuondoka katika makaazi yao huku mvua kubwa ikinyesha na kusababisha viwango vya maji kuongezeka kwa kasi, wakionekana kubeba mizigo yao kichwani na kupita katika maeneo yaliyofurika kwa maji. Awali Ijumaa, naibu gavana wa eneo hilo, Hassan Ibrahim Abdulle, alisema watu watatu wamekufa kutokana na mafuriko. Maafa hayo yanatokea baada ya ukame mkali kabisa kuwaacha mamilioni ya Wasomali kwenye hali mbaya ya njaa, huku taifa hilo pia likipambana na makundi ya uasi kwa miongo kadhaa.