Mahakama Kuu Tanzania yabariki mkataba wa bandari
10 Agosti 2023Kesi hiyo ambayo hukumu yale imesomwa leo, na jopo la majaji watatu ilivuta hisia za wengi hasa kutokana na suala hilo la mkataba kuiteka sehemu kubwa ya mijadala nchini humo.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Dastan Ndunguru amesema jopo la majaji watatu limesikiliza kwa kina hoja zote sita zilizoletwa na walalamikaji na hatimaye kujiridhisha kwamba hoja hizo zimekosa mashiko.
Amesema kwa msingi huo mkataba baina ya serikali na kampuni ya DP World hauna dosari za kufanya ushindwe kutekelezwa. Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na walalamikaji wanne ambao walidai mkataba huo unaenda kinyume na matakwa ya Katiba.
Jaji Ndunguru amesema “Licha ya athari za utaratibu lakini tunajizuia kuona kama upungufu huo uliathiri mkataba huo. Mahakama inajizuia kuvuka mipaka yake. Hivyo hoja hii pia mahakama imekataa.”
Soma pia: HRW waikosowa Tanzania kukandamiza wakosoaji
Baadhi ya hoja zilizotolewa na walalamikaji hao ni pamoja na mkataba wa IGA uliosainiwa na pande hizo mbili kukiuka sheria za nchi, mkataba kuridhiwa bila kuutoa kwa umma, huku wananchi wakikosa kushirikishwa kikamilifu.
Ama mambo mengine yaliyoletwa mbele ya mahakama hiyo ni pamoja na mkataba kuwa kinyume na maslahi ya umma na rasilimali za umma na mkataba kuhatarisha usalama wa nchi kwa baadhi ya vifungu.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari baada ya shauri hilo kutupiliwa mbali wakili wa walalamikaji Boniface Mwabukusi amesema timu yake inajipanga kusonga mbele kukata rufaa kuupinga uamuzi huo.
Kumekuwa na mjadala mkubwa unaogubika suala hilo tangu lilipojitokeza kwa umma na uamuzi huo wa mahakama unatarajiwa kuendelea kuwa sehemu ya mijadala hiyo ambayo tayari imewagawa wanasiasa wenye mirengo inayotofautiana.
Soma pia:CCM yatafsiriwa kuanza kubadili msimamo kuhusu makataba wa bandari
Kwa hivi sasa kumeanza kushuhudiwa hisia mseto kutokana na maamuzi hayo ya mahakama na baadhi wanasema wataendelea kuunga mkono juhudi za wanasheria kusonga mbele katika mahakama ya rufani.
Ama, mijadala pia katika majukwaa ya kisiasa inatarajiwa kuchukua mkondo mwingine wakati chama tawala CCM ambacho kimekuwa kikiupigia debe mkataba huo, kikitarajiwa kuendelea kukosoana na chama kikuu cha upinzani Chadema ambacho wanasiasa wake wamekuwa wakizunguka majukwani kuupinga mkataba huo.