Maiti ya Mugabe yawasili Harare
11 Septemba 2019Mjane wa Mugabe, Grace na makamo wa rais Kembo Mohadi ni miongoni mwa watu waliofuatana na maiti ya rais huyo wa zamani ndani ya ndege iliyotokea Singapore. Rais Mnangwagwa, maafisa wa ngazi ya juu wa serikali na familia ya Mugabe ndio waliopokea maiti ya rais huyo wa zamani katika uwanja wa ndege.
Umati wa watu walikusanyika katika uwanja huo wa ndege wa kimataifa masaa kadhaa kabla ya maiti kuwasili baadhi yao wakivalia mashati yenye picha ya Mugabe na wengine yenye picha za rais Mnangagwa huku muziki ukihanikiza kupitia vipaza sauti.
Mara baada ya kuwasili maiti ya Mugabe imepelekwa moja kwa moja katika kijiji chake cha Kutama, katika mkoa wa Zvimba magharibi ya mji mkuu Harare kwaajili ya ibada ya mazishi itakayodumu usiku kuchaa.
Wananchi wapatiwa fursa ya kumpa heshima za mwisho Mugabe
Kesho alkhamisi na pia siku ya ijumaa mwili wake utasafirishwa hadi uwanja wa michezo wa Rufaro katika kitongoji cha Mbare mjini Harare ili kuwaruhusu raia kutoka kila pembe ya nchi hiyo wampe hishma za mwisho. Uwanja huo wa michezo ndiko Mugabe alikoapishwa katika sherehe zilizofana za kukabidhiwa madaraka na waziri mkuu wa kikoloni Ian Smith.
Mazishi rasmi yatafanyika jumamosi katika uwanja wa taifa wa michezo ambako viongozi wa kigeni ikiwa ni pamoja na rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, rais Xi Jinping wa China na kiongozi wa zamani wa Cuba Raul Castro wanatarajiwa kuhudhuria.
Bado haijulikanai Mugabe atazikwa katika kiunga gani
Jamaa yake mmoja anasema kwa mujibu wa desturi za watu wa kabila la shona, machifu wa wa jadi kutoka Zvimbi ndio watakaokuwa na usemi wa mwisho kuhusu wapi akazikwe Robert Mugabe. Mazishi hasa ya Mugabe yamepanagwa jumapili ingawa bado haijulikani atazikwa wapi.
Familia yake na serikali ya rais Emmerson Mnangagwa wanaonekana wanazozana kama akazikwe kijijini kwao kaskazini magharibi mwa mji mkuu au katika kiunga cha mashujaa wa ukombozi mjini Harare.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga